Al-Azhar yaunga mkono ukarabati wa Gaza bila ya kuondolewa wakazi wake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122704-al_azhar_yaunga_mkono_ukarabati_wa_gaza_bila_ya_kuondolewa_wakazi_wake
Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar nchini Misri kimetoa mwito kuungwa mkono misimamo ya Misri na mataifa mengine ya Kiarabu katika ujenzi na ukarabati mpya wa Ukanda wa Gaza bila ya kuondolewa wakazi wake.
(last modified 2025-02-13T23:05:43+00:00 )
Feb 13, 2025 23:05 UTC
  • Al-Azhar yaunga mkono ukarabati wa Gaza bila ya kuondolewa wakazi wake

Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar nchini Misri kimetoa mwito kuungwa mkono misimamo ya Misri na mataifa mengine ya Kiarabu katika ujenzi na ukarabati mpya wa Ukanda wa Gaza bila ya kuondolewa wakazi wake.

Taarifa ya al-Azhar imesisitiza kuwa, inaunga mkono kwa dhati suala la kuijenga na kuikarabati Gaza, kwa sharti kwamba Wapalestina wasalie katika eneo hilo na kuongezwa mashinikizo ya kutekelezwa makubaliano ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.

Taasisi hiyo ya kidini ya Misri aidha imewataka viongozi wote wa Kiarabu na Kiislamu kupinga mpango wa kuwafukuza Wapalestina, ambao imesema lengo lake kufuta kabisa kadhia ya  Palestina kwa kuwalazimisha Wapalestina kuondoka katika ardhi yao, ambayo wameishi kwa maelfu ya miaka.

Al-Azhar imesisitiza kuwa, kupuuza jamii ya kimataifa kuwaunga mkono wanyonge na wanaodhulumiwa kutaitumbukiza dunia nzima katika machafuko na kuigeuza kuwa msitu wa kweli ambapo wenye nguvu watakanyaga haki za wanyonge na wanaodhulumiwa.

Rais wa Marekani, Donald Trump, amekariri bila ya aibu pendekezo lake tata la kulinyakua na kulidhibiti eneo la Ukanda wa Ghaza, akisema amejitolea "kulinunua na kulimiliki" eneo hilo lililoharibiwa na vita.

Mnamo Februari 4, Trump alifichua katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika Ikulu ya White House nia ya nchi yake ya kuutwaa Ukanda wa Gaza baada ya kuwahamisha wakazi wake wote wa Palestina na kuwapeleka katika nchi nyingine. Mpango huo umepingwa kikanda na kimataifa.