Maonyesho ya "Qur'ani katika Macho ya Wengine" yafunguliwa Tunisia
(last modified Mon, 17 Feb 2025 04:34:37 GMT )
Feb 17, 2025 04:34 UTC
  • Maonyesho ya

Maonyesho ya "Qur'ani katika Macho ya Wengine" yamefunguliwa katika Maktaba ya Kitaifa ya Tunisia, na yataendelea hadi Aprili 30, kwa ushirikiano wa Taasisi ya Urithi wa Kitaifa na Taasisi ya Utafiti wa Kisasa wa Maghreb.

Maonyesho hayo yanalenga kuchunguza athari za Qur’ani Tukufu kwa fikra za kifalsafa, kidini na kitamaduni za Ulaya tangu Zama za Kati, kwa kuonyesha zaidi ya nakala 80 adimu za hati, baadhi zikiwa ni kutoka taasisi za Tunisia na nyinginezo kutoka makumbusho ya kimataifa.

Nakala ya kale ya Qur'ani Tukufu

Maonyesho hayo yanatoa mtazamo mpya wa jinsi Qur’ani inavyoshughulikiwa katika mitazamo ya Ulaya, iwe kwa tafiti za kitaaluma au duru za mijadala ya kitamaduni na kifikra.

Kwa mujibu wa Dr. Khaled Kashir, Mkurugenzi wa Maktaba ya Kitaifa ya Tunisia, maonyesho ya "Qur'ani Katika Macho ya Wengine" ambayo yataendelea hadi Aprili 30, yana ujumbe unaovuka mipaka ya jadi kati ya Mashariki na Magharibi na yanalenga kuangazia makutano ya kitamaduni kati ya Uislamu na Ulaya.

Maonyesho hayo pia yanaweka wazi harakati za kuhamishwa misahafu na maandiko ya Kiislamu baina ya nchi za  Kiarabu za kaskazini mwa Afrika na Ulaya, na yanaonyesha hati za kihistoria zinazotoa mwanga wa jinsi Qur’ani ilivyokuwa kiini cha mijadala ya kifikra barani Ulaya, katika Zama za Kati na zama za sasa.

Katika muktadha huo, Kashir amedokeza kwamba baadhi ya maandiko ya Kiislamu yaliporwa wakati wa uvamizi wa Wahispania nchini Tunisia mwaka 1535, ambapo Qur’ani nyingi na vitabu vya kisayansi vilisafirishwa kwa magendo hadi Ulaya kupitia mitandao ya kubadilishana utamaduni, hasa Uhispania, Ujerumani na Italia.