WHO: Uganda imeripoti kifo kingine cha Ebola
Shirika la Afya Duniani WHO likinukuu Wizara ya Afya ya Uganda limesema mgonjwa wa pili wa Ebola amefariki dunia katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, kifo hicho kinafanya idadi ya kesi za Ebola zilizothibitishwa mpaka sasa katika mripuko huu mpya nchini Uganda kufikia 10.
Kifo hicho cha mtoto wa miaka minne na nusu kimeripotiwa chini ya wiki mbili baada ya Uganda kutangaza kwamba imeweza "kudhibiti" mripuko wa hivi karibuni wa virusi vya Ebola aina ya Sudan, ambao ulithibitishwa na Wizara ya Afya mwishoni mwa Januari.
Uganda ilitangaza kuzuka tena kwa ugonjwa huo wa kuvuja damu, unaoambukiza haraka sana na mara nyingi kusababisha kifo mwezi Januari mwaka huu, baada ya kifo cha muuguzi wa kiume (32) katika Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa ya Mulago katika mji mkuu Kampala.
Ofisi ya WHO nchini Uganda iliandika jana jioni kwenye mtandao wa X kwamba, Wizara ya Afya ya Uganda imeripoti "kisa cha ziada (cha kifo cha Ebola) katika Hospitali ya Taifa ya Mulago cha mtoto wa miaka minne na nusu, ambaye aliaga dunia siku ya Jumanne.
Wizara hiyo ilisema mnamo Februari 18 kwamba, wagonjwa wote wanane wa Ebola waliokuwa chini ya uangalizi wameruhusiwa kwenda nyumbani, lakini watu wasiopungua 265 wamesalia chini ya karantini kali mjini Kampala na miji mingine miwili.
Dalili za Ebola ni pamoja na homa, maumivu ya kichwa na misuli. Virusi vya maradhi hayo huambukizwa kwa kugusana na kutangamana na muathiriwa.