Wanajeshi 11 wauliwa kaskazini mwa Niger
Wanajeshi wasiopungua 11 wameuawa kaskazini mwa Niger na wengine kadhaa wamejeruhiwa.
Vyanzo vya habari nchini Niger vimeripoti kuwa wanamgambo wanaodaiwa kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda wamewaua wanajeshi 11 katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo lililopo karibu na mpaka na Algeria.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Air Info, wanajeshi waliokuwa kwenye doria katika eneo la Ekade Malane walivamiwa na kundi la wapiganaji wenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda.
Utawala wa kijeshi wa nchi hiyo ya ukanda wa Sahel wa mwaka 2023 uliahidi kushughulikia maswala ya usalama wa nchi hiyo lakini hata hivyo machafuko bado yanaendelea ambapo ripoti zinasema watu 2400 wameuawa tangu 2023.
Niger na washirika wake Mali na Burkina Faso wanatarajiwa kuunda kikosi cha pamoja cha wanajeshi 5,000 ili kukabiliana na machafuko ya katika ukanda huo.
Kwa sasa Niger inakabiliana na changamoto za kiusalama zinazosababishwa na magenge ya kigaidi yanayoendesha shughuli zao kutokea nchi jirani, hususan Libya.
Hali imekuwa mbaya zaidi tangu mwaka 2011, wakati wa operesheni ya kijeshi iliyoongozwa na NATO ilipouangusha utawala wa Muammar Gaddafi huko Libya, na kuacha ombwe la usalama ambalo magenge ya kigaidi yanalitumia vibaya.
Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, ugaidi na uhalifu wa kupangwa na vurugu za makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha vimezidi kuwa tishio kwa usalama katika eneo la Sahel Afrika hadi pwani ya Afrika Magharibi.