Jordan yapinga juhudi za RSF za kuunda serikali nyingine nchini Sudan
Jordan imepinga juhudi zozote zinazoweza kuhatarisha umoja wa Sudan, ikiwa ni pamoja na jitihada za kuundwa serikali nyingine ambazo zinafanywa na wapinzani wa jeshi la Sudan na imesema kuwa jambo hilo linaweza kushadidisha tu mgogoro wa Sudan.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Jordan imemnukuuu msemaji wa wizara hiyo, Sufian Qudah akithibitisha tena uungaji mkono mkubwa wa Jordan kwa jitihada za kuupatia ufumbuzi wa amani mgogoro wa Sudan sambamba na kulinda usalama wa nchi hiyo, utulivu, umoja wa ardhi, mamlaka kamili na ustawi wa watu wake.
Kabla ya hapo pia, nchi za Misri na Saudi Arabia zilitangaza kupinga jaribio lolote la kuunda serikali nyingine sambamba na ile ya hivi sasa nchini Sudan.
Tarehe 22 mwezi ulioisha wa Februari, Vikosi vya Msaada wa Haraka, (RSF), pamoja na vyama vya siasa na makundi yenye silaha nchini Sudan walitia saini mkataba wa kisiasa mjini Nairobi, Kenya, wa kuunda serikali nyingine sambamba na iliyopo hivi sasa katika maeneo yanayodhibitiwa na RSF
Serikali ya Sudan ilipinga vikali jambo hilo na kuilalamikia mno Kenya kwa kuwa mwenyeji wa kikao hicho na kwa kuwa na msimamo mzuri na vikosi vya RSF.
Tarehe 20 Februari, Sudan ilimrejesha nyumbani balozi wake aliyekuweko Nairobi, Kamal Jabara, ili kupinga kushiriki serikali ya Kenya katika majadiliano ya kuunda serikali nyingine nchini Sudan.
Hata hivyo Kenya ilitetea uamuzi wake huo ikisema kuwa, kuandaa mikutano hiyo ni sehemu ya juhudi zake za kutafuta suluhisho la kudumu la kumaliza vita nchini Sudan kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.