Kenya inazungumza na Thailand juu ya kuwarejesha raia 64 waliokwama Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123448-kenya_inazungumza_na_thailand_juu_ya_kuwarejesha_raia_64_waliokwama_myanmar
Kenya inafanya mazungumzo na Serikali ya Thailand ili kufungua tena mpaka wa nchi hiyo na Myanmar, ikitaka kuwahamisha raia 64 wa Kenya waliookolewa hivi karibuni kutoka kwenye mitandao ya magendo ya binadamu nchini Myanmar.
(last modified 2025-03-03T10:57:26+00:00 )
Mar 03, 2025 10:57 UTC
  • Baadhi ya raia wa kigeni waliokwama Myanmar
    Baadhi ya raia wa kigeni waliokwama Myanmar

Kenya inafanya mazungumzo na Serikali ya Thailand ili kufungua tena mpaka wa nchi hiyo na Myanmar, ikitaka kuwahamisha raia 64 wa Kenya waliookolewa hivi karibuni kutoka kwenye mitandao ya magendo ya binadamu nchini Myanmar.

Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora wa Kenya, Musalia Mudavadi, amethibitisha kwamba kundi hilo limekwama mpakani na ni miongoni mwa raia wa kigeni zaidi ya 7,000 waliookolewa kutoka kwa makundi yenye silaha lakini hawakuweza kuvuka mpaka na kuingia Thailand tangu Februari 12, wakati kundi la kwanza la wahanga 260, wakiwemo Wakenya 23, liliporuhusiwa kuingia nchini humo.

Musalia Mudavadi

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imesema: "Kenya inashauriana na Serikali ya Thailand ili kivuko cha mpakani kifunguliwe tena kwa misingi ya kibinadamu na kuruhusu raia waliookolewa kuingia katika eneo la Thailand na kurejeshwa Kenya." 

Wizara hiyo imesema Balozi wa Kenya nchini Thailand amekuwa akiwasiliana kila siku na raia hao huku maafisa wakitafuta njia mbadala za kuwarudisha nyumbani.

Hali inazidi kuwa mbaya katika Jimbo la Karen nchini Myanmar, ambapo waathiriwa wamehifadhiwa kwa muda katika kambi za kijeshi. Upungufu mkubwa wa huduma za matibabu, maji safi, umeme na usafi wa mazingira pia unaripotiwa katika eneo hilo.