Umoja wa Mataifa: Watoto wa mwaka mmoja ni miongoni mwa waliobakwa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123484-umoja_wa_mataifa_watoto_wa_mwaka_mmoja_ni_miongoni_mwa_waliobakwa_sudan
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, watu wenye silaha wanabaka na kuwanyanyasa kingono watoto wenye umri hadi mwaka mmoja katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.
(last modified 2025-03-04T07:44:30+00:00 )
Mar 04, 2025 07:44 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Watoto wa mwaka mmoja ni miongoni mwa waliobakwa Sudan

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, watu wenye silaha wanabaka na kuwanyanyasa kingono watoto wenye umri hadi mwaka mmoja katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.

Unyanyasaji mkubwa wa kingono wa watu wengi umerekodiwa na kutumiwa kama silaha ya vita katika mzozo huo wa karibu miaka miwili.

Theluthi moja ya waathiriwa ni wavulana, ambao kwa kawaida wanakabiliwa na "changamoto” katika kuripoti uhalifu kama huo na kutafuta msaada wanaohitaji.

Taarifa ya UNIICEF inaeleza kuwa, ingawa kesi 221 za ubakaji dhidi ya watoto zimeripotiwa rasmi tangu kuanza kwa 2024, idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi.

Sudan ni nchi yenye uhafidhina katika jamii na hilo huzuia waathirika na familia zao kuzungumza juu ya ubakaji, kwa hofu ya kuadhibiwa na makundi yenye silaha.

Aidha Mfuko huo wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa unasema waathiriwa 16 wa unyanyasaji wa kingono walikuwa na umri wa chini ya miaka mitano, wakiwemo watoto wachanga wanne.

Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka 2023 kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF)  linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.