Waislamu DRC waendelea na Ramadhani chini ya wingu la vita na machafuko
(last modified Sun, 09 Mar 2025 06:48:01 GMT )
Mar 09, 2025 06:48 UTC
  • Waislamu DRC waendelea na Ramadhani chini ya wingu la vita na machafuko

Ibada za mwezi mtukufu wa Ramadhani zinaendelea kwa Waislamu wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC huku hali ya Waislamu wa Goma ikiwa ni tofauti mara hii na Ramadhani nyingine.

Mji huo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ulitekwa mwezi Januari na waasi wa M23 na kuzusha hofu kubwa. Baadhi ya ada na desturi za Ramadhani haziwezekani hivi sasa mjini humo kutokana na hofu iliyopo. 

Muislamu mmoja wa Goma aliyejitambulisha kwa jina la Ahmed Salim amesema: “Kwa sasa baadhi yetu wanakutana majumbani mwao tu. Ibada za usiku kama Sala za Tarawehe zinasaliwa kama kawaida Msikitini. Lakini si Waislamu wengi wanaokwenda kama ilivyokuwa zamani.

Ijumaa ya juzi Msikiti anaosali Ahmed Salim ulijaa Waislamu ambao walifurika Msikitini humo kumuomba Mwenyezi Mungu kuwaletea amani na kupunguza mauamivu yao. 

Muislamu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Maris Mambo amesema: "Mawaidha yote Misikitini yanahimiza amani. Tunalazimika kuwasiliana Waislamu kwa njia hii ya Sala za jamaa. Wakati wa mwezi huu wa Ramadhani tunaomba amani irejee kwenye jimbo letu na katika nchi nzima kwa ujumla. 

Hii ni mara ya kwanza kwa Waislamu wa Goma kupitisha mwezi mtukufu wa Ramadhani katika hali ngumu kama hii chini ya uvamizi wa waasi wa M23.

Viongozi wa jamii ya Kiislamu katika majimbo yaliyotekwa na waasi wa M23 wanawatuliza watu na kuwataka waasi hao kuwahakikishia waumini usalama wao katika kipindi chote hiki. 

Akizungumzia suala hilo, Imam Djuma Dauda amesema: “Viongozi wetu walikwenda kuwaona watu wapya wanaosimamia mji wa Goma. Namshukuru Mungu, walituletea ujumbe wa kututaka tusiwe na wasiwasi na tunaweza kusali Sala zetu za usiku tukiwa salama. Viongozi hawa wapya wametupa ruhusa na kuwataka Waislamu wawe watulivu na wasifanye ibada kwa sauti kubwa. Pia wawe wanavaa mavazi ya Waislamu ili watambuliwe kuwa wao ni Waislamu, wasishambuliwe."