Tanzania yatangaza kumalizika mlipuko wa Marburg
Tanzania jana Alkhamisi ilitangaza mwisho wa mlipuko wa virusi vya Marburg, kwani hakuna kesi yoyote mpya iliyoripotiwa nchini humo katika kipindi cha siku 42.
Charles Sagoe-Moses, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki amesema, "Wakati mlipuko huo umetangazwa kuwa umemalizika, tunasalia kuwa macho kujibu haraka ikiwa kesi yoyote itakayogunduliwa na tunaunga mkono juhudi zinazoendelea za kutoa huduma za kisaikolojia kwa familia zilizoathiriwa na mlipuko huo."
Habari zaidi zinasema kuwa, hakuna kesi mpya zilizoripotiwa katika muda wa siku 42 zilizopita, baada ya kifo cha kesi ya mwisho iliyothibitishwa mnamo Januari 28.
Jumla ya watu 10 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kesi mbili zilizothibitishwa na zinazowezekana nane, kulingana na WHO.
Mlipuko huo katika mkoa wa kaskazini magharibi mwa Kagera ulitangazwa mnamo Januari 20, baada ya mlipuko wa kwanza kuripotiwa katika eneo hilo hilo mnamo 2023.
Januari mwaka huu, Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) kilitangaza kuhamasisha msaada wa haraka wa kuisaidia Tanzania kukabiliana na mripuko huo wa virusi vya Marburg.
Kabla ya hapo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alilishukuru shirika la WHO kwa kuchukua hatua za dharura kudhibiti maradhi hayo.