RSF yaua na kujeruhi makumi ya raia wa Sudan Kordofan Kusini
(last modified Thu, 03 Apr 2025 02:32:47 GMT )
Apr 03, 2025 02:32 UTC
  • RSF yaua na kujeruhi makumi ya raia wa Sudan Kordofan Kusini

Kwa akali raia 12 wa Sudan wameuawa katika mashambulizi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika Jimbo la Kordofan Kusini.

Waasi wa RSF na mshirika wao Sudan People's Liberation Movement-North (SPLM-N) walitumia silaha nzito kushambulia maeneo ya makazi katika jimbo hilo la kusini mwa Sudan, ambapo makumi ya watu wamjeruhiwa pia.

Mtandao wa Madaktari wa Sudan ulisema hayo kwenye mtandao wa kijamii wa X jana Jumatano na kuongeza kwamba, mamia ya familia pia zimelazimika kukimbia makazi yao kutoka na mashambulio hayo katika eneo la Khor al-Dalib, yaliyoanza tangu Jumatatu.

Kadhalika vyanzo vya ndani vya Sudan vimeripoti kwamba, mapigano yanaendelea kati ya jeshi la Sudan na RSF magharibi mwa Al-Obeid, mji mkuu wa Jimbo la Kordofan Kaskazini, huko katikati mwa Sudan. 

Wakati huo huo, duru za kiusalama zinaarifu kuwa, jeshi la Sudan linapiga hatua mpya kusini mwa El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, na kwamba wapiganaji wa RSF wameshambulia sehemu ya magharibi ya mji huo kwa mizinga.

Ramani inayonesha jimbo la Kordofan Kusini, kusini mwa Sudan

Wiki iliyopita, jeshi la Sudan lilisema kuwa limesafisha mabaki ya RSF mjini Khartoum, baada ya kurejesha udhibiti wa uwanja wa ndege wa mji mkuu, makao makuu ya usalama, na vitongoji kadhaa vya mashariki na kusini kwa mara ya kwanza tangu Aprili 2023.

Tangu Aprili 2023, jeshi la Sudan na vikosi vya RSF vimekuwa katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 20,000 na kuibua mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi na njaa, huku takriban Wasudan milioni 15 wakilazimiika kuhama makazi yao.