Maelfu ya Wamisri waandamana Sinai kuiunga mkono Palestina
(last modified Wed, 09 Apr 2025 13:42:34 GMT )
Apr 09, 2025 13:42 UTC
  • Maelfu ya Wamisri waandamana Sinai kuiunga mkono Palestina

Maelfu ya wananchi wa Misri kutoka majimbo mbalimbali wamekusanyika karibu na Uwanja wa Ndege wa El-Arish katika Mkoa wa Sinai Kaskazini wakitangaza kuunga mkono kadhia ya Palestina na kupinga jaribio lolote la kuwafurusha Wapalestina kutoka katika ardhi zao.

Huku wakipeperusha bendera za Misri na Palestina, waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango yaliyosomeka "Hapana kwa kuhamisha" na "Tunasimama na Gaza," miongoni mwa jumbe nyinginezo,  wametangaza kuunga mkono mpango wa ujenzi mpya wa Gaza uliopendekezwa na Misri.

"Tunaunga mkono kadhia ya Palestina na haki za Wapalestina, dhidi ya majaribio ya kuhamishwa kwao na (Waziri Mkuu wa Israel Benjamin) Netanyahu na (Rais wa Marekani Donald) Trump," Soad Mostafa, ambaye anatoka jimbo la Port Said na mwanachama wa Chama cha Watetezi wa Nchi, ameliambia shirika la habari la Xinhua wakati wa maandamano hayo.

Maandamano hayo ya Jumanne yalifanyika wakati Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alipotembelea mji wa Arish kwenye mpaka wa Misri na Gaza, ambapo Misri inapokea misaada ya ndani na kimataifa kuelekea Gaza iliyozingirwa kupitia kivuko cha Rafah. Hospitali za Arish pia zinatibu makumi ya Wapalestina waliojeruhiwa.

Macron aliwasili Cairo Jumapili jioni kwa ziara ya siku tatu. Siku ya Jumatatu, Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi, Macron, na Mfalme Abdullah II wa Jordan walifanya mkutano wa pande tatu huko Cairo, ambapo walitoa taarifa ya pamoja ya kutaka kufufuliwa mara moja mapatano ya usitishaji vita huko Gaza.