Algeria yawapa wanadiplomasia wa Ufaransa saa 48 waondoke nchini humo
(last modified Mon, 14 Apr 2025 13:09:49 GMT )
Apr 14, 2025 13:09 UTC
  • Algeria yawapa wanadiplomasia wa Ufaransa saa 48 waondoke nchini humo

Mvutano wa kidiplomasia kati ya Algeria na Ufaransa umezidi kupamba moto huku serikali ya Algiers ikiwataka wanadiplomasia 12 wa mkoloni huyo wa zamani wa Ulaya kuondoka nchini humo ndani ya saa 48.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noël Barrot amesema leo Jumatatu kwamba, Algeria imewataka wanadiplomasia hao wa Ufaransa kuondoka nchini humo kufuatia kukamatwa kwa raia watatu wa Algeria nchini Ufaransa.

Kwa miongo kadhaa, uhusiano kati ya Algeria na Ufaransa umepitia misukosuko kadhaa ya kidiplomasia, na tangazo la leo Jumatatu linakuja wakati nyeti katika uhusiano na linaonyesha ugumu katika kurekebisha uhusiano.

"Ninaziomba mamlaka za Algeria kuachana na hatua hizi za kufukuza (wanadiplomasia)," Barrot amesema na kuongeza, "Ikiwa uamuzi wa kuwarudisha maafisa wetu utadumishwa, hatutakuwa na chaguo lingine ila kujibu mara moja."

Kabla ya hapo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria ilimwita balozi wa Ufaransa mjini Algiers, Stephane Romatet ili kujieleza; ikiwa ni kuonesha malalamikio makali ya Algiers kuhusu kuzuiliwa balozi mdogo wa Algeria nchini Ufaransa.

Juzi Jumamosi, serikali ya Ufaransa ilimweka kizuizini kwa muda balozi wa Algeria kwa madai ya kuhusishwa na tukio la mwaka 2024 la kutekwa nyara Amir Boukhras, mwanaharakati aliyekuwa anasakwa wa Algeria aliyekuwa anaishi Paris na ambaye ni maarufu kwenye mitandao ya kijamii kwa jina la "AmirDZ."

Algeria imetaka kuachiliwa huru mara moja balozi wake huyo, ikionya kwamba vitendo kama hivyo vya serikali ya Paris vinadhooofisha juhudi za hivi karibuni za kurejesha uhusiano wa pande mbili, ikiwa ni pamoja na makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo ya simu kati ya viongozi wakuu wa nchi hizo mbili.