Wanajeshi 70 wa Benin wauawa katika shambulio la kigaidi
(last modified Sun, 20 Apr 2025 12:56:26 GMT )
Apr 20, 2025 12:56 UTC
  • Wanajeshi 70 wa Benin wauawa katika shambulio la kigaidi

Kundi la kigaidi la Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda limetangaza kuwa wapiganaji wake wameua wanajeshi 70 katika mashambulizi dhidi ya vituo viwili vya kijeshi kaskazini mwa Benin.

Hayo yamesemwa na shirika la ujasusi la SITE na kuongeza kuwa: Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya mauaji yaliyofanywa na magaidi wa JNIM nchini humo, na katika zaidi ya muongo mmoja wa shughuli zake katika eneo la Afrika Magharibi.

Taifa hilo la Afrika Magharibi na jirani yake wa pwani ya Togo yamekumbwa na mfululizo wa mashambulizi ya kigaidi katika miaka ya hivi karibuni.

Mashambulizi haya yanafanyika huku makundi yenye uhusiano na ISIS na al-Qaeda yakipanua uwepo wao zaidi ya eneo la Sahel kuelekea kaskazini.

Magaidi wa Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) 

Benin na mataifa mengine ya Ghuba ya Guinea, Togo na Ivory Coast zinashuhudia kuongezeka kwa mashambulio yanayofanywa na wanamgambo wenye uhusiano na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na Daesh, wakati ghasia hizo zikiongezeka kuelekea upande wa kusini kutoka kanda ya Sahel Afrika.

Makumi ya maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni 3 wakilazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi tangu kundi la Boko Haram lianzishe hujuma zake nchini Nigeria mwaka 2009.