Serikali ya CAR yatangaza mazungumzo na upinzani miezi michache kabla ya uchaguzi wa urais
Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imetangaza kuwa, inataka kufanya mazungumzo ya kisiasa na mrengo wa upinzani ikiwa ni miezi michache kabla ya uchaguzi wa urais mwezi Desemba mwaka huu.
Taarifa za azma ya serikali ya kufanya mazungumzo na wapinzani imethibitishwa na Fidèle Gouandjika, mshauri wa karibu wa rais Faustin-Archange Touadéra.
Ingawa Rais Faustin-Archange Touadéra anasema kwa sasa anaangazia masuala ya nchi, ugombeaji wake wa kuchaguliwa tena hauonekani kuwa wa shaka. Hiki ndicho upinzani unakataa, na umetangaza kuandaa maandamano mapya.
Katika hotuba aliyoitoa wakati wa kuadhimisha miaka minne ya muhula wake wa pili, rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati alitangaza kwamba "anaungana na kambi ya Jamhuri kutetea katiba" ili "kuimarisha amani kwa njia ya mazungumzo."
Kwa mujibu wa mshauri maalum wa Mkuu wa Nchi, Fidèle Gouandjika, wajumbe wa serikali, pamoja na "taasisi nyingine za jamhuri" watawajibika kuendesha mazungumzo haya. Lakini "tunasubiri BRDC itoe hoja wanazotaka kushughulikia ili serikali iweze kuanza kazi," Fidèle Gouandjika ametuambia.
Upinzani unapinga vikali uwezekano wa muhula wa tatu wa Faustin-Archange Touadéra.
Maelfu ya waandamanaji walimiminika katika mitaa ya Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Aprili 4 mwezi huu wakiandamana bega kwa bega na wabunge wa upinzani kupinga vikali taarifa kwamba Rais Faustin-Archange Touadéra wa nchi hiyo anafanya juhudi za kuwania kiti cha urais kwa muhula wa tatu.