Meja Jenerali Salami: IRGC haitasalimu amri mkabala wa adui yeyote
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema kuwa jeshi hilo la SEPAH kamwe halitarudi nyuma na kusalimu amri mbele ya maadui wa Iran.
Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema IRGC iliundwa kwa ajili ya kupata ushindi, na katu haitarudi nyuma dhidi ya adui yeyote.
Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Walimu jana Jumapili hapa Tehran, Meja Jenerali Salami ameieleza IRGC kuwa shirika la kipekee na la aina yake hapa nchini.
"IRGC ni taasisi ambayo inahitajika katika kudumisha mawazo ya nguvu, dhamira na ubunifu ili kuelewa vyema mabadiliko ya mazingira," ameongeza Meja Jenerali Salami.
Kamanda Salami amesisitiza kuwa, nguvu za kijeshi za Iran na historia yake pana zinalifanya taifa hili lisiweze kutetereshwa na mashinikizo ya maadui.
Amebainisha kuwa, IRGC inapaswa kugundua mawazo ya adui na kutabiri hatua zao, ili iweze kuzizima. Kamanda wa Jeshi la IRGC la Iran amesisitiza kuwa, tishio lolote litakalotekelezwa dhidi ya Iran litakabiliwa na jibu zito na la maangamivu.