IRGC yasema iko tayari kujibu uchokozi wowote wa adui kwa nguvu zaidi
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limeonya kwamba, kitendo chochote kipya cha uadui dhidi ya Iran kitakabiliwa na jibu kubwa zaidi.
IRGC ilisema hayo katika taarifa yake jana Alkhamisi, kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kujiri Operesheni ya Ahadi ya Kweli 2, shambulio la kisasi la makombora la Jeshi la Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Taarifa hiyo imeonya kwamba, hesabu yoyote mpya isiyo sahihi au uchokozi kutoka kwa Israel utakabiliwa na jibu zito, sahihi zaidi, na mbaya zaidi kuliko hapo awali.
IRGC imeonyesha mafanikio ya uwezo wa makombora na ndege zisizo na rubani za Iran, na kubainisha kuwa zilifanikiwa kupenya mifumo ya ulinzi ya tabaka nyingi ya Israel.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, operesheni hiyo ilionyesha uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu wa kupiga kwa "usahihi wa kustaajabisha," na kuifanya mifumo ya ulinzi ya Israel kukosa ufanisi dhidi ya silaha za hali ya juu za Iran.
IRGC imesisitiza kuwa, hatua yoyote tarajiwa ya Israel dhidi ya Iran itakabiliwa na ulipizaji kisasi wa wa kujutisha na utakaousogeza utawala haramu wa Kizayuni karibu zaidi na kuporomoka kwake.
Iran ilivurumisha makombora yasiyopungua 200 ya balestiki katika vituo vya kijeshi na usalama vya Israel mnamo Oktoba 1, 2024, wakati wa Operesheni ya Ahadi ya Kweli ya 2 ili kuuadhibu utawala wa Israel kwa kumuua kiongozi wa kisiasa wa Harakati ya Muqawama ya Hamas, Ismail Haniyeh mjini Tehran na kiongozi wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah huko Beirut, pamoja na mauaji ya watu huko Gaza na Lebanon.