IRGC: Adui hana ubavu wa kuanzisha vita vipya dhidi ya Iran
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema Israel na washirika wake hawana uwezo wala ubavu wa kuanzisha vita vipya dhidi ya Iran, hivyo basi, wamekimbilia operesheni za vita vya kisaikolojia.
"Adui hawezi kuanzisha vita vipya, lakini anataka kuiweka nchi katika anga inayofanana na ya vita, iliyojaa taharuki na mvutano," ameeleza Brigedia Jenerali Ali Mohammad Naeini na kuongeza kuwa, "Kwa madhumuni haya, inafuatilia operesheni za kisaikolojia. Sisi hatuanzishi vita, na wala hatuviogopi."
Msemaji wa Jeshi la SEPAH ameeleza bayana kuwa, "Tunawaambia wananchi wa Iran wasiwe na wasiwasi; iwapo vita vitaibuka, sisi ndio tuliyoshikilia mpini, na tuna nguvu ya kujihami ambayo itamfanya adui kujuta."
Brigedia Jenerali Ali Mohammad Naeini amekumbusha kuwa, baada ya vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na maadui wa Iran mnamo Juni 13, tarehe 24 Juni, Jamhuri ya Kiislamu kupitia operesheni zake za kulipiza kisasi zilizofanikiwa dhidi ya utawala wa Israel na Marekani, ilifanikiwa kusimamisha uchokozi huo wa kigaidi.
Naeini amesema, doktrini ya usalama ya Israel iliporomoka wakati wa vita hivyo na kusisitiza kuwa, utawala huo ulikosea kwenye mahesabu juu ya nguvu ya Iran, na kuamini kimakosa kwamba Wairani wangesalimu amri baada ya shambulio la awali. Badala yake, amesema, "watu (wa Iran) walitoa jibu la kuponda dhidi ya adui mwenye njozi."
Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, vita hivyo vilidhihirisha umoja wa taifa la Iran, nguvu ya wanajeshi, na ufanisi wa uongozi wa nchi hii. Ameongeza kuwa, Iran iliibuka "imara zaidi, na yenye mshikamano na nguvu" baada ya uchokozi huo wa siku 12 wa Marekani na Israel.