Iran yalaani shambulio dhidi ya Port Sudan lililoua mamia ya watu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani shambulizi la ndege isiyo na rubani ambalo lililenga uwanja wa ndege pamoja na maeneo na vituo vya kiraia mashariki mwa Sudan.
Katika taarifa ya jana Jumapili, Esmaeil Baqaei amelaani shambulizi hilo la ndege isiyo na rubani ambalo limelenga uwanja wa ndege na vituo vya kiraia vya mji wa bandari wa Port Sudan, mashariki mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Aidha ameeleza wasiwasi wake kuhusu kuendelea kwa mashambulizi ya kijeshi kwenye vituo vya kiraia na manispaa ya Sudan, kama vile mitambo ya kuzalisha umeme, hospitali, mitambo ya kusafisha maji, na viwanja vya ndege visivyo vya kijeshi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mashambulizi dhidi ya raia na maeneo ya kiraia nchini Sudan.
Akielezea wasiwasi wake kuhusu janga kubwa la njaa na wimbi la watu waliokimbia makazi yao nchini Sudan, Baqaei ametoa wito kwa jamii ya kimataifa na mashirika ya kiraia kutekeleza wajibu wao na kukomesha mapigano nchini Sudan, na vile vile kufanikisha juhudi za kupekwa misaada ya kibinadamu kwa watu wa taifa hilo la Kiarabu.
Hapo jana, Msemaji wa jeshi la Sudan alitangaza kuwa wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka RSF walifanya shambulio la droni katika kambi ya jeshi la nchi hiyo na katika vituo vingine karibu na uwanja wa ndege wa Port Sudan.
Hilo lililkuwa shambulio la kwanza kuwahi kufanywa na wanamgambo wa RSF katika mji huo wa bandari wa mashariki mwa Sudan.