Jeshi la Msumbiji laokoa wanawake 280 na watoto kutoka mikononi mwa wanamgambo wa Naparama
Jeshi la Msumbiji limesema kuwa limefanikiwa kuokoa wanawake na watoto wasiopungua 280 waliokuwa wametekwa nyara na wanamgambo wa Naparama katika majimbo ya kaskazini na katikati mwa nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Afrika.
Brigedia Jenerali Bernado Ntchokomola, ambaye inasemekana ndiye aliyeongoza operesheni ya uokoaji, amewaambia waandishi wa habari kwamba watu hao walikuwa wanashikiliwa kwa zaidi ya wiki mbili msituni katika jimbo la Zambezia.
Amesema: "Wahanga walikuwa wakipewa mafunzo na watekaji nyara tayari kuandikishwa katika kikundi cha wanamgambo. Na wanawake walikuwa wakibakwa mara kwa mara na watekaji nyara huku watoto na waume zao wakisubiri wazazi wao bila ya matumaini ya kupata msaada wowote."
Ameongeza kkuwa, wahanga hao waliookolewa sasa watarudishwa kwenye jamii zao lakini bado wanaishi kwenye mazingira ya hofu ambayo wahalifu hao wameyaunda.
Naparama ni kundi la wanamgambo ambalo liliibuka wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 16 vilivyodumu tangu mwaka 1977 hadi 1992.
Kwa mujibu wa maafisa wa jeshi, wanachama wa genge hilo wanapewa mafundisho ya "ibada" maalumu ambazo huwafanya wajihisi kuwa ni watu wenye ulinzi usio wa kawaida ambao hakuna cha kuwadhuru.
Katika miezi ya hivi karibuni, polisi nchini Msumbiji wameripoti kutokea mashambulizi ya genge hilo la wahalifu katika maeneo mbalimbali ya majimbo ya katikati na kaskazini mwa nchi hiyo.