Maelfu waliokimbia vita Sudan wanarejea nchini kutoka Misri
Makumi ya maelfu ya Wasudani waliolazimika kuhama makazi yao kutokana na vita sasa wanarejea nchini licha ya vita kuendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya Sudan.
Karibu Wasudani milioni 13 walikimbia vita vya ndani huku milioni nne kati yao wakielekea katika nchi jirani na waliosalia wakipewa hifadhi katika maeneo mbalimbali nchini humo.
Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa baadhi ya raia wa Sudan wameanza taratibu kurudi nchini na kwamba idadi ya watu wanaorudi Sudan kutoka nchi jirani inaongezeka. Wasudani wasiopungua milioni 1 na laki tano walikimbilia Misri mara baada ya kuibuka vita nchini kwao. Walid Abu al Seid, mratibu wa usafiri unaotumiwa na wakimbizi hao wa Sudan amesema kuwa huko Cairo mamia ya Wasudani wanapanda mabasi mawili au matatu kila siku na kurejea nyumbani.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limeeleza kuwa, takriban Wasudani 123,000 wamerejea kutoka Misri tangu kuanza kwa mwaka huu.
Shirika hilo linakadiria kuwa, wakimbizi 400,000 waliopewa hifadhi ndani ya Sudan wamerejea majumbani mwao katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu Khartoum, katika jimbo la karibu la al Gezira na katika jimbo la Sennar. Pamoja na hayo lakini, aghalabu ya raia hao wa Sudan wanaorejea nyumbani wamekuta makazi yao yameharibiwa na vita wakisalia bila huduma ya umeme, chakula, maji na huduma nyinginezo.