Mapigano yapamba moto Kivu Kusini huko DRC; mazungumzo ya amani yakwama
Mapigano yaliripotiwa kutokea jana Jumatatu katika jimbo la Kivu Kusini la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, licha ya kwamba mazungumzo baina ya serikali na waasi wa M23 yanaendelea nchini Qatar.
Walioshuhudia wamesema kuwa, kundi moja la vijana wa kujitolea wanaoungwa mkono na jeshi la Kongo lilishambuliwa na waasi wa Twirwaneho na Red Tabara, ambao wanashirikiana na kundi la waasi wa M23 kwenye eneo la milima la Fizi lenye utajiri mkubwa wa maliasili.
Mkazi moja wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Maulidi Mtoca amesema: "Ilikuwa ni Twirwaneho ndio waliokuja kushambulia wazalendo na wanajeshi wa Kongo hapa... Wanachoma nyumba, na mapigano yamekuwa yakiendelea tangu saa 12 asubuhi."
Ghasia hizo zimeripuka wakati Rais wa Kongo Felix Tshisekedi akiwa amekubali kuketi katika meza ya mazungumzo na waasi wa M23 ili kutafuta njia za kutatua migogoro ya nchi hiyo. Hata hivi sasa wajumbe kutoka pande zote mbili wako mjini Doha Qatar kwa mazungumzo ya amani.
Licha ya pande zote mbili kutoa taarifa za kutaka kusitishwa mapigano, lakini vita vinaendelea katika maeneo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri, huku waasi wa M23 wakizidi kuteka vijiji na miji kutoka mikononi mwa wanajeshi wa serikali.
Juzi Jumapili, waasi wa M23 waliuteka mji wa Lunyasenge kwenye ufuo wa magharibi wa Ziwa Edward mashariki mwa Kongo. Mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu 17 wakiwemo wanajeshi saba wa DRC.