Mjumbe wa Trump: Mazungumzo ya Iran na Marekani ni chanya
Mjumbe wa rais wa Marekani, Donald Trump katika ukanda wa Asia Magharibi amesema kuwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani ni chanya, na kwamba juhudi zinaendelea za kuhakikisha inafanyika duru nyingine ya mazungumzo hayo mwishoni mwa wiki hii.
Akizungumza mjini Washington, D.C. leo Jumanne, Steve Witkoff amesema kuwa: "Naona tunaelekea upande sahihi. Rais anataka kuona hili likitatuliwa kidiplomasia ikiwezekana, kwa hivyo tunafanya kila tuwezalo kulifanikisha."
Mjumbe huyo wa Trump ametoa maelezo zaidi akisema, mazungumzo hayo yaliyoanza kwa upatanishi wa Oman mjini Muscat na kisha Roma Italia na duru ya tatu kufanyika tena Muscat, yanaweza kuingia kwenye duru ya nne mwishoni mwa wiki. Awali duru ya nne ya mazungumzo hayo ilikuwa imepangwa kufanyika Mei 3 katika mji mkuu wa Italia, lakini, iliakhirishwa.
Witkoff amesema, haipaswi kuchukuliwa hatua yoyote itakayopelekea kuchelewa kuingia kwenye duru nyingine ya mazungumzo hayo. Amesema pia kwamba wiki ijayo rais wa Marekani atafanya ziara ya kuzitembelea nchi za Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Nchi za Kiarabu na Qatar.
Mjumbe huyo wa Trump amerejea madai ya kila siku ya kwamba wanataka kuizuia Iran isimiliki silaha za nyuklia, wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran muda wote imekuwa ikitangaza kwamba, silaha za nyuklia hazimo kabisa katika mikakati yake ya kiulinzi. Si hayo tu lakini pia usalama wa mradi wa nyuklia wa Iran umethibitishwa mara nyingi tu na kwa namna ya kipekee na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Wakala huo umekuwa ukitangaza mara kwa mara kwamba haujawahi kupata ushahidi wowote wa kuonesha kuwa, mradi wa nyuklia wa Iran umetoka kwenye mkondo wake wa amani na wa masuala ya kiraia.