Mazungumzo ya amani ya Kongo-Rwanda: Rasimu yawasilishwa
Kongo na Rwanda zimewasilisha rasimu ya pendekezo la amani kama sehemu ya mpango wa kumaliza mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo.
Mzozo huo uliongezeka mapema mwaka huu wakati waasi wa M23 "wanaoungwa mkono na Rwanda" walipoteka miji muhimu ya Kongo, ikiwemo Goma na Bukavu.
Mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 7,000 na kuwafanya wakimbizi zaidi ya watu milioni 7. Mgogoro wa mashariki mwa DRC ni moja ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani.
Eneo la mashariki mwa Kongo lina utajiri mkubwa wa madini muhimu kama vile kobalti, dhahabu na shaba. Pendekezo la amani linaonekana kama njia ya kufungua uwekezaji mkubwa wa kigeni katika sekta ya madini ya nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda amesema kuwa mazungumzo ya makubaliano ya mwisho ya amani yataendelea baadaye mwezi huu, huku kukiwa na matumaini kwamba marais wa Rwanda na Kongo watatia saini makubaliano hayo ifikapo katikati ya mwezi Juni mwaka huu katika sehere ambayo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa kikanda na kimataifa.
Rasimu ya pendekezo la amani inafuatia mkutano wa mwezi Aprili ambapo Kongo na Rwanda ziliahidi kufanyia kazi makubaliano ya amani ya kumaliza vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.