UNHCR: Wakimbizi wa Sudan wanaoingia Chad wanaongezeka
(last modified Wed, 07 May 2025 07:12:46 GMT )
May 07, 2025 07:12 UTC
  • UNHCR: Wakimbizi wa Sudan wanaoingia Chad wanaongezeka

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR, limeelezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la wakimbizi wa Sudan wanaoingia katika nchi ya Chad.

Taarifa ya UNHCR imeeleza kuwa, takriban watu 20,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wamekimbilia Chad katika wiki mbili zilizopita kutokana na kuongezeka ghasia na mapigano katika jimbo la Darfur hasa kwenye mji wa El-Fasher, na kusisitiza kuwa kuongezeka kwa idadi hiyo kumezua hali ya kutisha mpakani.

Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa, katika kipindi cha wa wiki tatu zilizopita, zaidi ya raia 540 wamethibitishwa kuuawa huko Darfur Kaskazini, huku vita kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF vikiendelea kusababisha maafa makubwa na sasa vikiwa vimepamba moto katika mji wa Port-Sudan.

Tangu Aprili 15, 2023, RSF imekuwa ikipigana na jeshi kwa udhibiti wa Sudan, hali ambayo imesababisha maelfu ya vifo na kuibua moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya Wasudani 20,000 wameuawa na wengine milioni 15 wamelazimika kuhama tangu vita vianze. Serikali ya Sudan inatuhumu Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kuunga mkono kundi la waasi wa RSF linalotekeleza uhalifu wa mauaji ya kimbari nchini humo.

Wakati huo huo, Serikali ya Sudan ilitangaza jana Jumanne kwamba imeamua kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kumrejesha nyumbani balozi wake, ikitangaza kuwa Imarati ni "nchi chokozi."