Israel yaendeleza ukatili Gaza, yaua shahidi Wapalestina wengine 33
(last modified Mon, 12 May 2025 12:00:34 GMT )
May 12, 2025 12:00 UTC
  • Israel yaendeleza ukatili Gaza, yaua shahidi Wapalestina wengine 33

Wapalestina wasiopungua 33 wameuawa shahidi katika muda wa saa 24 zilizopita huko Gaza, maafisa wa afya katika eneo hilo lililo chini ya mzingiro wameripoti.

Wizara ya Afya ya Palestina imeripoti hayo leo Jumatatu na kuongeza kwamba, Wapalestina wengine zaidi ya 90 huko Gaza pia wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel ndani ya saa 24 zilizopita.

Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, "Idadi kubwa ya waathiriwa imesalia chini ya vifusi na barabarani, kwa kuwa hawawezi kufikiwa na ambulensi na wafanyakazi wa ulinzi wa raia." 

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, idadi ya wahanga wa hujuma hizo za kikatili za Wazayuni tangu Machi 18 mwaka huu mpaka sasa imefikia mashahidi 2,749 na majeruhi 7,607.

Haya yanajiri wakati Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) likieleza kuwa, hali ya kibinadamu huko Gaza ni janga lisiloweza kufikirika.

"Mashambulio ya anga, vizuizi na njaa vinaendelea, na makumi ya maelfu ya watu wameuawa na kujeruhiwa," UNRWA imesema kwenye ujumbe wake uliotumwa kwenye mtandao wa X.

Kadhalika shirika linalofuatilia takwimu za njaa duniani (IPC) limesema: Wakazi wote wa Gaza wako katika hatari kubwa ya baa la njaa, na kwamba Wapalestina nusu milioni katika eneo hilo wanawajihiwa na kifo kutokana na makali ya njaa.