Watu wasiojulikana waua watu 12 na kujeruhi 17 Sudan Kusini
(last modified Mon, 12 May 2025 05:44:24 GMT )
May 12, 2025 05:44 UTC
  • Watu wasiojulikana waua watu 12 na kujeruhi 17 Sudan Kusini

Kundi la watu wasiojulikana wenye silaha wameua takriban watu 12 na kujeruhi wengine 17 huko Sudan Kusini mapema jana Jumapili.

Hayo yameripotiwa na vyombo vya habari vya ndani ambayo vimesema: "Washambuliaji walivamia vijiji vya eneo hilo yapata saa 7 usiku na kufyatua risasi ovyo wakati watu wakiwa wamelala.

William Koji, Kaimu Waziri wa Habari wa Jimbo la Ziwa, amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, shambulio hilo la kushitukiza limepelekea watu wasiopungua 12 kuuawa huku wasichana wawili na watoto wadogo wawili wakiwa miongoni mwa watu waliouawa.

Kwa upande wake shirika la habari la Aweil limemnukuu kaimu huyo wa waziri wa habari wa Jimbo la Ziwa la Sudan Kusini akisema kuwa, washambuliaji hao wanashukiwa kuwa ni vijana wenye silaha kutoka kaunti jirani za jimbo la Unity, na walivamia ili kuipa idadi isiyojulikana ya ng'ombe, lakini baadhi ya ng'ombe wamepatikana kwa msaada wa jeshi la Sudan Kusini.

Akilaani shambulio hilo, William Koji ameitaka serikali ya jimbo la Unity kuchukua hatua za kukomesha vitendo vya wahalifu kuvamia mifugo na hasa ng'ombe na kuua raia wasio na hatia.

Amesema: "Hii ni mbaya sana, na ninawaomba wenzetu kutoka Jimbo la Unity kuwashughulikia wahalifu hawa kwa sababu hatukuweza kuvuka kutoka Jimbo la Ziwa kwenda Jimbo la Unity ili kuwakamata."