Je, tishio jipya kwa amani ya Ethiopia ni nini?
Uamuzi wa serikali ya Ethiopia wa kufuta hadhi ya kisheria ya Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) umeibua wasiwasi mkubwa kuhusu mustakabali wa amani nchini humo.
Hatua hii inachukuliwa huku athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya chama hicho na serikali ya shirikisho zikiwa bado hazijatatuliwa kikamilifu, huku wakazi wengi wa Tigray wakiendelea kukumbwa na matatizo yanayotokana na vita.
Makubaliano ya Amani Yanayoweza Kuvunjika
Kwa miongo kadhaa, TPLF imekuwa na nafasi muhimu katika siasa za Ethiopia, ikiongoza serikali baada ya kuanguka kwa utawala wa kijeshi mnamo 1991 hadi ilipoondolewa madarakani mwaka 2019 kufuatia kuingia madarakani kwa Waziri Mkuu Abiy Ahmed. Mgogoro baina ya TPLF na serikali ya sasa hatimaye ulisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wa Tigray mnamo 2020, vita vilivyodumu hadi Novemba 2022 na kumalizika kufuatia makubaliano ya amani ya Pretoria.
Tume ya Uchaguzi ya Ethiopia imeamua kufuta usajili wa TPLF kwa sababu ya kutofanya mkutano mkuu wa chama, lakini hatua hii ina athari kubwa kisiasa na kijamii. Chama hicho ni sehemu ya serikali ya muda ya Tigray na kina jukumu muhimu katika utekelezaji wa makubaliano ya amani ya Pretoria. Viongozi wa chama wanasema kuwa hatua hii inahatarisha uhalali wao na inaweza kudhoofisha makubaliano ya amani.

Uamuzi huu unaweza kuchochea mvutano mpya kati ya vikosi vya Tigray na serikali ya shirikisho, kwani malalamiko ya kisiasa hayajatatuliwa na utekelezaji wa vipengele vya makubaliano ya amani unakabiliwa na changamoto nyingi. Moja ya masuala makubwa ni kurejea wakimbizi wa vita, jambo ambalo bado halijatekelezwa kikamilifu na linaweza kuwa gumu zaidi kutokana na hali mpya.
Baada ya tangazo la tume ya uchaguzi, TPLF imeomba Umoja wa Afrika kuingilia kati na kuishinikiza serikali ya shirikisho kusitisha utekelezaji wa marufuku hiyo.
Onyo kwa Serikali ya Ethiopia
Chama hicho kimetoa tahadhari kuwa hatua hii inaweza kuhatarisha mchakato wa amani. Mataifa kadhaa yameelezea wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mvutano eneo la Tigray. Weledi wa kisiasa wanaonya kuwa kurejea kwa ghasia nchini Ethiopia kunaweza kuwa na athari mbaya kwa eneo zima la Pembe ya Afrika.
Kwa kuzingatia hali ya sasa, haijulikani ni kwa kiwango gani serikali ya shirikisho itakuwa tayari kujibu au kutekeleza matakwa ya TPLF. Kutofikiwa makubaliano kunaweza kuongeza mvutano wa ndani na kuathiri utekelezaji wa makubaliano ya amani.
Wakati jumuiya ya kimataifa inaendelea kusisitiza umuhimu wa kuendeleza mchakato wa amani, hali ya ndani ya Ethiopia bado ni tete. Marufuku hii haijaathiri tu hatima ya TPLF, bali inaweza kuwa na athari pana kwa mazingira ya kisiasa na kijamii nchini Ethiopia. Mustakabali wa amani nchini humo utategemea kiwango cha mazungumzo kati ya pande husika na kwa msingi huo ni jukumu la Umoja wa Afrika kupatanisha pande hasimu ili kuhakikisha kuwa nchi hiyo, ambayo mji wake mkuu, Addis Ababa, ni makao makuu ya umoja huo inapata uthabiti na amani endelevu.