Waziri Mkuu wa zamani wa Chad aendelea kushikiliwa korokoroni
Mahakama moja nchini Chad imeamuru kurejeshwa rumande na kuendelea kushikiliwa korokoroni, Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Succès Masra.
Francis Kadjilembaye, wakili wa Masra, amesema kuwa kesi ya mteja wake ilisikilizwa na wakili wa serikali na kisha kuchunguzwa na hakimu kabla ya kuwekwa kizuizini kabla ya kufunguliwa kesi rasmi.
"Kesi itaanza kusikilizwa mara jaji husika atakapopatikana," amesema Kadjilembaye mbele ya waandishi wa habari katika mji mkuu wa Chad, N'Djamena.
Masra alikamatwa wiki iliyopita ili kufanyiwa uchunguzi wa madai ya kuchochea chuki na uadui ndani ya umma. Hayo ni kwa mujibu wa Oumar Mahamat Kedelaye, mwanasheria mkuu wa nchi hiyo.
Kedelaye amesema kukwa, uchunguzi uliofanywa na polisi umefichua kuhusika Masra katika tuhuma zinazomkabili kupitia ujumbe mbalimbali wa chuki aliosambaza kwenye mitandao ya kijamii wakiwataka watu kujizatiti katika mapigano makali ya wafugaji na wakulima ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 40 katika jimbo la kusini mwa nchi la Logone Occidental.
Masra, ambaye pia ni mkuu wa chama cha upinzani cha The Transformers, alienda uhamishoni mwaka 2022 lakini baadaye alirejea nchini Chad na kuteuliwa kuwa waziri mkuu na Rais Mahamat Idriss Deby Itno. Baada ya kuhudumu kama waziri mkuu kwa miezi mitano mwaka 2024, Masra alijiuzulu ili kutoa nafasi ya kuundwa serikali mpya.