Libya yafunga bomba la mafuta karibu na mji wa Zawiya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i126792-libya_yafunga_bomba_la_mafuta_karibu_na_mji_wa_zawiya
Shirika la Taifa la Mafuta la Libya (NOC) linalomilikiwa na serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa limetangaza kuwa limelazimika kufunga bomba la mafuta baada ya kugundua kupasuka na kuvuja mafuta huko kusini mwa Zawiya, yapata kilomita 45 magharibi mwa mji mkuu Tripoli.
(last modified 2025-05-25T03:21:00+00:00 )
May 25, 2025 03:21 UTC
  • Libya yafunga bomba la mafuta karibu na mji wa Zawiya

Shirika la Taifa la Mafuta la Libya (NOC) linalomilikiwa na serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa limetangaza kuwa limelazimika kufunga bomba la mafuta baada ya kugundua kupasuka na kuvuja mafuta huko kusini mwa Zawiya, yapata kilomita 45 magharibi mwa mji mkuu Tripoli.

Katika taarifa yake, NOC imesema kuwa, timu zake za matengenezo na dharura zinafanya kazi kudhibiti uvujaji kama ambavyo imetoa amri ya kusitishwa mara moja uzalishaji wa mafuta kwenye visima vya Hamada baada ya kugunduliwa tatizo hilo.

Hatua mbalimbali zimechukuliwa mbali na hizo ili kupunguza mashinikizo kwenye bomba hilo. Timu ya wataalamu pia inafanya uchunguzi wa kubaini sababu zilizopelekea kuvuja mafuta ya bomba hilo ili iweze kujulikana ni uchakavu tu wa bomba au ni tukio la uhalifu.

Eneo hilo la uzalishaji mafuta ni katika maeneo ambayo makundi hasimu yenye silaha huko nyuma yalikuwa yakibadilishana udhibiti wake mara kwa mara kwa kutumia mtutu wa bunduki.

Mapigano ya uchu wa madaraka baina ya makundi hasimu nchini Libya yamepelekea kutoshughulikiwa ipasavyo miundombinu mingi ikiwemo ya kuzalisha na kusafirisha mafuta. 

Mwezi Agosti 2020, Mkuu wa Bodi ya Shirika la Taifa la Mafuta nchini Libya alitahadharisha kuwa maafa makubwa yalikuwa yanainyemelea Libya kutokana na kusitisha uuzaji nje mafuta ya nchi hiyo na kurundikwa bidhaa hiyo katika maghala kutokana na vita baina ya makundi hasimu. 

Alisema, ongezeko la makundi yenye silaha na kuwepo vifaru na maghala mengi yaliyojaa mafuta katika bandari za mafuta za Libya ni mambo ambayo yalikuwa yanazidisha hatari ya kutokea maafa makubwa na miripuko ya kutisha nchini humo.