Afrika Kusini yaadhimisha Siku ya Afrika kwa mwito wa umoja na ushirikiano
(last modified Mon, 26 May 2025 10:22:33 GMT )
May 26, 2025 10:22 UTC
  • Afrika Kusini yaadhimisha Siku ya Afrika kwa mwito wa umoja na ushirikiano

Afrika Kusini jana Jumapili iliadhimisha Siku ya Afrika kwa mwito wa kusisitizia umoja na ushirikiano wa kikanda na mshikamano wa kiutamaduni kwenye bara zima.

Katika sherehe za kitaifa zilizofanyika kwenye Hifadhi ya Uhuru mjini Pretoria ambalo ni eneo lililoteuliwa la urithi, Naibu Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini, Peace Mabe, alitoa mwito wa kufanyika juhudi zaidi za kufikia ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu ya bara zima la Afrika.

Siku ya Afrika, inayoadhimishwa Mei 25 kila mwaka, ni kumbukumbu ya kuanzishwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1963, ambao sasa unajulikana kwa jina la Umoja wa Afrika (AU).

Katika hotuba yake, Mabe alisisitiza kwa kusema, bara la Afrika lina uwezo mkubwa wa kiuchumi na kiutamaduni, akitoa mwito kwa mataifa ya Afrika kuimarisha uhusiano baina yao kupitia biashara, umoja wa lugha na mshikamano wa kihistoria.

Vilevile alitilia mkazo mapambano ya pamoja ya bara zima la Afrika dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi. "Historia yetu ya pamoja ya kupiga vita ukoloni na ubaguzi wa rangi pia inatuleta pamoja," alisema.

Lengo la Siku ya Afrika ni kusherehekea umoja, amani na tofauti za kitamaduni barani Afrika. Wakati huo huo, mashirika ya kiraia, mashirika ya haki za binadamu na vyama vya wafanyakazi vilishiriki katika Matembezi ya Mshikamano ya Siku ya Afrika huko Johannesburg siku ya Jumamosi.

Matembezi hayo yalianzia Mary Fitzgerald Square huko Newtown hadi Constitution Hill huko Braamfontein, yakiashiria safari inayoendelea ya kupigania haki, uhuru na ushirikiano wa Afrika nzima.