Rais wa Sudan Kusini amfuta kazi Jaji Mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu
(last modified Fri, 30 May 2025 03:04:15 GMT )
May 30, 2025 03:04 UTC
  • Rais wa Sudan Kusini amfuta kazi Jaji Mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amemfuta kazi Jaji Mkuu wa muda mrefu aliyekuwa pia Mkuu wa Mahakama ya Juu, Chan Reec Madut pamoja na naibu wake John Gatwech Lul.

Hayo yametangazwa na Shirika la Utangazaji la Sudan Kusini (SSBC) linalomilikiwa na serikali. Salva Kiir pia amemteua Benjamin Bak Deng kuchukua nafasi ya Madut, na Laku Trankilo Nyumbi kuwa naibu wa Jaji Mkuu. Kiongozi huyo wa Sudan Kusini hakutoa sababu ya kufutwa kazi Madut na naibu wake.

Madut aliteuliwa na Salva Kiir mwezi kushika nafasi hiyo mwezi Agosti 2011, muda mfupi baada ya Sudan Kusini kujitenga na ardhi nyingine ya Sudan mwezi Julai mwaka huo. Deng, jaji mkuu mpya, ni jaji mwenye uzoefu ambaye alihudumu nchini Sudan katika nyadhifa tofauti kwa miaka kadhaa kabla ya Sudan Kusini kujitenga na ardhi nyingine za Sudan.

Hadi kuteuliwa kwake Jumatano, Deng alikuwa mkurugenzi wa mafunzo na utafiti na pia mjumbe wa Mahakama ya Juu ya Sudan Kusini. Naibu wake mpya Nyumbi alikuwa mkurugenzi wa Masuala yanayohusiana na majaji kama ambavyo alikuwa pia mjumbe wa Tume ya Huduma ya Mahakama, ambayo inasimamia shughuli za mahakama zote za Sudan Kusini.

Kufutwa kazi Madut kumekuja huku kiongozi wa upinzani na Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar akiendelea kutumikia kifungo cha nyumbani tangu Machi 26 mwaka huu wa 2025.

Tangu Sudan Kusini ilipojitenga na ardhi nyingine za Sudan mwezi Julai 2011 hadi hivi sasa, haijawahi kuwa na utulivu wa kutegemewa hata mara moja. Hata baada ya Riek Machar kujiunga na serikali, bado hali ni tete Sudan Kusini.