Mafuriko yaua makumi ya watu nchini Nigeria
(last modified Sat, 31 May 2025 02:21:31 GMT )
May 31, 2025 02:21 UTC
  • Mafuriko yaua makumi ya watu nchini Nigeria

Makumi ya watu wamepoteza maisha huku maelfu ya wengine wakilazika kuhama makazi yao kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha nchini Nigeria.

Timu za waokoaji nchini humo zinaendelea kuopoa miili baada ya kujiri mafuriko hayo yaliyosababisha vifo vya takriban watu 36 katika maeneo mbali mbali ya nchi.

Kwa mujibu wa maafisa wa dharura, mvua hizo kubwa zimesababisha vifo vya watu 25 katika Jimbo la Rivers lenye utajiri mafuta, kusini mwa Nigeria.

Habari zaidi zinasema kuwa, mvua kubwa zinazonyesha nchini humo zimesomba zaidi ya nyumba 50 katika jimbo la Niger, kaskazini ya kati. 

Mafuriko hayo yamesababisha maelfu ya watu kuhama makazi yao, na yameharibu au kuathiri mamia ya nyumba na mashamba yaliyokuwa na mazao ya kilimo.

Mwaka jana, malaki ya watu walipoteza maisha na wengine zaidi ya 740,000 walilazimika kuhama makazi yao nchini Nigeria, kutokana na mafuriko yaliyokumba maeneo mengi ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Nigeria mara nyingi hukabiliwa na mafuriko ya msimu, lakini mipango duni ya miji, mifumo duni ya mabomba ya maji taka, na mabadiliko ya tabianchi yanafanya majanga hayo kuwa ya mara kwa mara na kusababisha vifo.