Wasomi Nigeria: Falsafa ya Imam Khomeini ni kuwa, uongozi unatokana na watu
(last modified Mon, 02 Jun 2025 06:45:08 GMT )
Jun 02, 2025 06:45 UTC
  • Wasomi Nigeria: Falsafa ya Imam Khomeini ni kuwa, uongozi unatokana na watu

Wasomi nchini Nigeria wamesisitiza kuwa, alama kuu ya kumbukumbu na urithi wa Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomein (MA) ni msimamo wake kuwa mamlaka na nguvu za uongozi zipo mikononi mwa wananchi.

Profesa Dauda Nalado wa Chuo Kikuu cha Aminu Kano cha Nigeria katika mahojiano na Iran Press amesema, ushawishi wa kudumu wa falsafa ya Imam Khomeini unatokana na namna alivyosisitiza kwamba nguvu ya kweli iko kwa watu, hasa vijana, na wala si mikononi mwa watawala madhalimu.

Ameeleza bayana kuwa, miongo kadhaa baada ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, fikra za Imam Khomeini (MA) zinaendelea kuhamasisha harakati za kimataifa za uadilifu na kujitawala.

Msomi huyo mashuhuri wa Nigeria ameeleza bayana kuwa, falsafa ya Imam Khomeini kuwa mamlaka ipo mikononi mwa watu, imechagiza harakati za vijana na midahalo ya kisiasa duniani kote.

Hapo jana, Jumuiya ya Azzahra nchini Nigeria, kwa ushirikiano na Chuo cha Al-Mustapha cha Kano na Jukwaa la Kitaaluma la Harakati ya Kiislamu ziliandaa kongamano mjini Kano, kaskazini mwa Nigeria, kwa ajili ya kutafakari maisha na mchango wa Imam Khomeini (MA).

Akizungumza katika mkutano huo, Profesa Abdullahi Danladi, Mkuu wa Jukwaa la Rasilimali la Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ameeleza namna kipindi cha kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, wanafunzi wa Nigeria walivyokuwa wameathiriwa kwa kiasi kikubwa na mitindo ya maisha ya Kimagharibi, kujitenga na mafundisho ya Kiislamu; lakini baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, Jumuiya ya Wanafunzi wa Kiislamu ya Nigeria (MSSSN) ilituma ujumbe, ukiongozwa na Sheikh Zakzaky, kwenda Iran mwaka 1979.

Amesema kurudi kwao na kueneza ujumbe wa Imam Khomeini kuliibua shauku mpya katika mafundisho ya Kiislamu miongoni mwa vijana wa Nigeria.