UN yaelezea hofu yake kuhusu haki za binadamu Libya
(last modified Fri, 06 Jun 2025 06:48:12 GMT )
Jun 06, 2025 06:48 UTC
  •  UN yaelezea hofu yake kuhusu haki za binadamu Libya

Umoja wa Mataifa umetaka uchunguzi huru ufanyike kuhusu mauaji ya kiholela yanayodaiwa kufanywa na kundi lenye silaha la Libya kufuatia kupatikana makumi ya maiti kwenye makaburi ya umati katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Miili hiyo imepatikana katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi la SSA ambalo ni moja ya vikundi vya wanamgambo wenye nguvu sana mjini Tripoli. Kundi hili lilizusha vita na kundi jingine mjini Tripoli baada ya kuuawa kiongozi wake, Abdel-Ghani al-Kikli mwezi uliopita wa Mei.

Al-Kikli, anayejulikana pia kwa jina la "Gheniwa," alikuwa miongoni mwa makamanda wa wanamgambo wenye ushawishi mkubwa wa mjini Tripoli na alikabiliwa na shutuma za kufanya mauaji ya kiholela na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Wanamgambo wa SSA wanahusishwa na Baraza la Rais na serikali inayotambuliwa kimataifa huko Tripoli kama kikosi cha usalama.

Kabla ya kifo chake, al-Kikli alikuwa ameingia kwenye mzozo na makundi mengine yenye silaha.

Mauaji yake yalisababisha mapigano ya silaha katika mji mkuu, ambayo ni mabaya zaidi kuwahi kutokea tangu Agosti 2023, wakati makundi hasimu mjini Tripoli yalipopigania udhibiti wa mji mkuu huo na kusababisha vifo vya watu 55.

Kufuatia ghasia hizo, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHR) imesema kuwa, miili 10 iliyoungua vibaya iligunduliwa katika makao makuu ya SSA kwenye kitongoji cha Abu Salim, huku miili 67 zaidi ikipatikana kwenye majokofu katika hali tofauti za kuoza kwenye hospitali za Abu Salim na Al Khadra.

Kaburi jingine linaloshukiwa kuwa la umati limeripotiwa kugunduliwa katika mbuga ya wanyama ya Tripoli inayoendeshwa na wanamgambo wa SSA.

Volker Turk, kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kugunduliwa maiti hao kumezidisha hofu ya kuweko mauaji mabaya zaidi ambayo Umoja wa Mataifa hauna taarifa nayo na huo ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na kundi hilo la SSA huko Tripoli, mji mkuu wa Libya.