Iran iko tayari kusaidia Kenya kujenga nyumba milioni moja
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i127310-iran_iko_tayari_kusaidia_kenya_kujenga_nyumba_milioni_moja
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa tayari kuisaidia Kenya kujenga nyumba milioni moja za bei nafuu nchini humo.
(last modified 2025-06-08T01:04:20+00:00 )
Jun 08, 2025 01:04 UTC
  • Iran iko tayari kusaidia Kenya kujenga nyumba milioni moja

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa tayari kuisaidia Kenya kujenga nyumba milioni moja za bei nafuu nchini humo.

Hayo yamedokezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uendelezaji Miji ya Iran, Bw. Abdolreza Golpayegani akiwa safarini nchini Kenya kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat) uliofanyika hivi karibuni jijini Nairobi.

Bw. Golpayegani, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Barabara na Maendeleo ya Miji nchini Iran, amekutana na Waziri wa Ardhi, Ujenzi wa Umma, Nyumba na Maendeleo ya Miji wa Kenya, Bi. Alice Wahome, ambapo wamejadili uwezekano wa ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya makazi, hususan kwenye nyumba za bei nafuu.

Katika mazungumzo hayo, Bi. Wahome ameeleza jitihada za serikali ya Kenya katika miaka mitano iliyopita za kujenga angalau nyumba 200,000 kila mwaka kwa lengo la kufikia jumla ya nyumba milioni moja, akibainisha kuwa mpango huo unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma, binafsi na wawekezaji wa kimataifa.

Aidha, Waziri huyo amesisitiza kuwa Kenya ina uhitaji mkubwa wa vifaa vya msingi vya ujenzi kama saruji, chuma na vifaa vya usafi wa majumbani huku akitaja mahitajio hayo kama fursa ya biashara ya kuagiza bidhaa hizo kutoka Iran.

Kwa upande wake, Bw. Golpayegani ametaja uhusiano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili kuwa msingi imara wa kuendeleza ushirikiano wa kimaendeleo. Amesisitiza kuwa Iran iko tayari kushirikisha kampuni zake zenye uwezo mkubwa katika kusaidia Kenya kutimiza azma yake ya kutoa makazi bora kwa wananchi kupitia mpango wa nyumba za bei nafuu.

Rais William Ruto wa Kenya mara kadhaa amesisitiza azma ya serikali yake ya kuwajengea wananchi wa matabaka ya chini nyumba za bei nafuu ili waweze kuishi kwa hadhi. Katika kutekeleleza mpango huo kivitendo hivi karibuni Rais Ruto alikabidhi nyumba 1,080 za gharama nafuu kwa wakazi wa Mukuru Kwa Njenga Jijini Nairobi.