UN yapongeza uamuzi wa Libya wa kushughulikia masuala ya usalama
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) umekaribisha uamuzi wa Baraza la Uongozi la Libya wa kuunda kamati mbili za kushughulikia masuala ya usalama na haki za binadamu kufuatia mapigano ya hivi karibuni ya silaha katika mji mkuu Tripoli.
"Juhudi hizi zinalenga kuimarisha usalama na kuzuia kuzuka mapigano na kuhakikisha raia wako salama. Aidha kushughulikia masuala ya haki za binadamu magerezeni ikiwa ni pamoja na kuondoa kuwekwa watu kizuizini kiholela," imesema taarifa ya UNSMIL.
Siku ya Alkhamisi Baraza la Uongozi la Libya lilichukua uamuzi wa kuunda kamati ya kufanya mipango ya usalama na kijeshi huko Tripoli. Vilevile liliunda kamati nyingine yenye jukumu la kufuatilia hali ya haki za binadamu ndani ya vituo vya mahabusu na magereza, pamoja na kuorodhesha na kupitia upya kesi zilizotolewa hukumu bila ya uangalizi mzuri wa mahakama.

Mvutano ulizuka mjini Tripoli katikati ya mwezi uliopita wa Mei baada ya kuzuka mapigano makali kuzuka kati ya kundi la wanamgambo la SSA lenye nguvu mjini Tripoli na Brigedi ya 444. Makundi yote hayo mawili yanadaiwa kuiunga mkono serikali ya Waziri Mkuu wa Libya Abdul-Hamid Dbeibah inayotambuliwa kimataifa. Vurugu hizo zilianza baada ya kuuawa kamanda wa SSA ndani ya kituo kinachodhibitiwa na Brigedi ya 444.
Libya imekuwa imekumbwa na mgawanyiko wa kisiasa na ukosefu wa usalama tangu ulipoangushwa utawala wa kiongozi wa zamani Kanali Muammar Gaddafi mwaka wa 2011. Watawala wapye wa Libya wameshindwa kudhibiti hali ya mambo nchini humo, huku makundi mengi yenye silaha yakiendesha shughuli zao kwa uhuru.