Kundi la Wagner latangaza kuondoka Mali baada ya zaidi ya miaka 3
Kampuni binafsi ya kijeshi ya Russia maarufu kwa jina la Wagner imetangaza kuwa imeamua kuondoka nchini Mali, na hivyo kumaliza zaidi ya miaka mitatu ya operesheni zake katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Wagner imesema kwenye taarifa yake ya mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba: "Dhamira imekamilika" na "PMC Wagner inarejea nyumbani."
"Tulisaidia wazalendo wa ndani kuunda jeshi dhabiti na lenye nidhamu ambalo sasa lina uwezo wa kulinda ardhi yao. Miji mikubwa yote ya mikoa ya Mali imerejea kwenye udhibiti wa serikali halali," imesema taarifa ya kundi hilo.
Pia taarifa hiyo imesema: "Tumeua maelfu ya wanamgambo na makamanda wao ambao walikuwa wanatishia usalama wa raia kwa miaka mingi."
Mali, ni nchi iliyoko katika eneo la Sahel la barani Afrika na imekuwa ikishuhudia vitendo vya waasi tangu mwaka 2012. Wanajeshi nchini humo waliiomba Russia kulisaidia taifa la Mali baada ya kuvunja uhusiano na mkoloni Ufaransa na washirika wengine wa Magharibi.
Ripoti zinasema kuwa licha ya tangazo hilo la Wagner, lakini Russia itaendelea kuwepo katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi pamoja na "Jeshi la Afrika" yaani kikosi cha Russia kinachosimamiwa na serikali.
Mapema mwaka huu, nchi za Mali, Burkina Faso na Niger, zilizokuwa chini ya utawala wa kijeshi, zilijiondoa rasmi katika jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi ECOWAS. Nchi hizo tatu zimeunda kambi yao zenyewe inayoitwa, Muungano wa Mataifa ya Sahel.