Wafadhili walaani mashambulizi dhidi ya raia nchini Sudan
(last modified Sun, 08 Jun 2025 06:18:39 GMT )
Jun 08, 2025 06:18 UTC
  • Wafadhili walaani mashambulizi dhidi ya raia nchini Sudan

Nchi 30 wafadhili duniani zimelaani mashambulizi dhidi ya raia na wafanyakazi wa masuala ya kibinadamu nchini Sudan na kutaka mashambulio hayo yakomeshwe mara moja.

Usiku wa tarehe pili mwezi huu wa Juni, kulitokea shambulio dhidi ya msafara wa misaada ya kibinadamu wa malori 15 wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF huko Al Koma, kaskazini mwa Darfur, magharibi mwa Sudan.

Itakumbukwa kuwa mashambulio hayo yalisababisha vifo vya watu watano wa msafara huo na kujeruhi wengine kadhaa. Malori manne kati ya 15 ya msafara huo yaliharibiwa katika shambulio hilo na mengine matano yalipata uharibifu wa kiasi fulani.

"Malori hayo yalikuwa yamebeba takriban tani 100 za lishe muhimu, vifaa vya afya, elimu na mahitaji mengine ambayo yalikusudia kusaidia watoto na familia katika mji wa El Fasher," imesema taarifa hiyo.

Zikisisitiza kwamba kulengwa kwa makusudi wafanyakazi wa masuala ya kibinadamu ni ukiukaji wa sheria za kimataifa, nchi wafadhili zimesisitiza kwamba raia na wafanyakazi wa masuala ya kibinadamu wanapaswa kuheshimiwa na wasihusishwe na mashambulizi ya pande hasimu. 

Taarifa hiyo pia imerejelea mwito wake kwa makundi mawili hasimu yaani SAF na RSF wa kukomesha mara moja uhasama na kuzingatia majukumu yao mbele ya sheria za kimataifa zinazohusiana na masuala ya kibinadamu.