Mwanajeshi wa Uingereza aliyembaka mwanamke Kenya akamatwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i127356-mwanajeshi_wa_uingereza_aliyembaka_mwanamke_kenya_akamatwa
Mwanajeshi wa Uingereza anayehudumu katika kambi ya mafunzo ya kijeshi nchini Kenya amekamatwa kwa tuhuma za kumbaka mwanamke.
(last modified 2025-06-09T03:20:31+00:00 )
Jun 09, 2025 03:20 UTC
  • Mwanajeshi wa Uingereza aliyembaka mwanamke Kenya akamatwa

Mwanajeshi wa Uingereza anayehudumu katika kambi ya mafunzo ya kijeshi nchini Kenya amekamatwa kwa tuhuma za kumbaka mwanamke.

Tukio hilo liliripotiwa tokea mwezi uliopita, baada ya kundi la wanajeshi kutembelea baa moja katika mji wa Nanyuki, karibu na kambi ya mafunzo ya kijeshi ya Uingereza inayojulikana kama BATUK (British Army Training Unit Kenya).

Uchunguzi wa kina unaendeshwa na Kitengo Maalum cha Makosa Mazito cha Wizara ya Ulinzi ya Uingereza, ambacho hushughulikia kesi kubwa zinazohusiana na wanajeshi wa Uingereza ndani na nje ya nchi.

Haya yanajiri wakati ambao mwaka jana, jeshi la Uingereza lilianzisha uchunguzi kuhusu mienendo ya wanajeshi waliotumwa kwenye kambi hiyo kufuatia madai mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mauaji ya mwanamke mwaka 2012.

Mwili wa Agnes Wanjiru, mama wa mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 21, ulipatikana ndani ya tanki la majitaka katika hoteli ya Lions Court mjini Nanyuki miezi miwili baada ya kuripotiwa kutoweka mnamo Machi 2012.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti la The Sunday Times, mwanajeshi mmoja wa Uingereza aliyetuhumiwa kwa mauaji hayo alitajwa na wenzake baada ya kudaiwa kujigamba kutekeleza mauaji hayo.

Wanajeshi wa Uingereza walioko Kenya kwa mafunzo chini ya mpango wa BATUK kwa zaidi ya nusu karne wanakabiliwa na tuhuma nzito za ubakaji, mauaji na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya wanawake na watoto wanaoishi karibu na kambi zao. Aidha wanajeshi hao wa Uingereza wameharibu mazingira ya maeneo wanayofanyia mazoezi nchini Kenya ambapo mbali na kuteketeza moto misitu pia wameacha nyuma idadi kubwa ya mabomu ambayo hayajalipuka. Kwa miongo kadhaa, mabomu hayo yaliyoachwa na jeshi la Uingereza yamejeruhi binadamu, mifugo na wanyamapori.

Aidha katika jinai nyingine, Jeshi la Uingereza linalofanya mazoezi nchini Kenya limekuwa likitumia silaha zenye kemikali hatari ya fosforasi (phosophorus) ambazo matumizi yake yamepigwa marufuku kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Silaha hizo hutumika karibu na makazi ya raia ambapo sasa wakazi wa eneo la Samburu kunakofanyika mazoezi hayo wana wasiwasi kuhusu athari mbaya za silaha hizo.