UN yalaani ukiukaji wa makubaliano ya amani Libya
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) umelaani ukiukaji wa mapatano ya amani katika mji mkuu, Tripoli, ambapo mapigano yalizuka mapema jana Jumatatu kati ya makundi hasimu yenye silaha wakati wa sherehe za sikukuu ya Idul Adh'ha.
Katika taarifa yake, UNSMIL imezitaka pande zote kuheshimu mapatano yaliyofikiwa na kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza kudhoofisha makubaliano hayo.
"Migogoro inapotokea katika maeneo ya mijini, uwezekano wa kuuawa raia huwa ni mkubwa sana," imesema taarifa hiyo na kutoa mwito kwa pande zote kuacha uchochezi na kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, limetaka wale wote waliohusika na mashambulizi dhidi ya raia huko Libya, wawajibishwe.
Walioshuhudia wamesema kuwa, mapigano yalizuka mapema jana Jumatatu kati ya makundi hasimu yenye silaha katika sehemu fulani za mji mkuu Tripoli, na kuzusha hofu miongoni mwa raia. Hakuna majeruhi walioripotiwa hadi hivi sasa.
Wizara ya Ulinzi ya Libya imethibitisha kutokea mapigano hayo na imesisitiza kuwa yamemalizika. Wizara hiyo imeyaonya makundi hasimu yasirejee kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano ikisisitiza tena kuwa kwake tayari kuchukua hatua muhimu za kuimarisha usalama.
Ghasia zinazuka mara kwa mara mjini Tripoli, ikiwa ni pamoja na mapigano makubwa ya mwezi uliopita kati ya vikosi vitiifu kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) inayotambuliwa kimataifa na Kitengo cha Kusaidia Kuleta na Kuimarisha Utulivu SSA ambacho ni kikundi kilichojizatiti kwa nguvu za silaha na ushawishi, katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.