Ajali mbaya ya barabarani Kenya, watu 33 wafariki dunia na kujeruhiwa
Watalii sita wamefariki dunia na wengine 27 wamejeruhiwa katika ajali iliyotokea kwenye barabara yenye magari mengi katikati mwa Kenya Jumatatu jioni. Hayo yamethibitishwa na afisa mmoja wa serikali wa eneo hilo.
Kamishna wa Kaunti ya Nyandarua Abdrisack Jaldesa amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, basi lililokuwa linawasafirisha watalii hao kutoka Kaunti ya Nakuru kuelekea Nyahururu Thomson Falls katika Kaunti ya Laikipia lilibiringia na kutua kwenye mtaro katika eneo la Gichaka, kwenye umbali wa kilomita 41 kusini mwa mji wa Nyahururu.
Jaldesa amesema kuwa, waliojeruhiwa wamepelekwa haraka katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Nyahururu na kuongeza kuwa utambulisho wa watalii hao bado haujajulikana.
Walioshuhudia wamesema kwamba, basi hilo lilikuwa likisafiri kando ya barabara huku mvua ikinyesha wakati dereva aliposhindwa kulidhibiti basi hilo na kuacha njia. Kisha gari hilo liligonga mti na kubiringia mara kadhaa, na kuua watu sita waliokuwemo ndani na kujeruhi wengine 27.
Wakaazi wa eneo hilo wamesema kuwa walikimbilia kwenye eneo la tukio na kuwaokoa manusura waliokuwa wamenasa ndani ya basi hilo.