Sudan Kusini kuanza zoezi la kuwapokonya silaha raia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i127404-sudan_kusini_kuanza_zoezi_la_kuwapokonya_silaha_raia
Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kuwa, inatarajia kuanza zozei la kuwapokonya silaha raia.
(last modified 2025-06-10T08:22:32+00:00 )
Jun 10, 2025 08:22 UTC
  • Sudan Kusini kuanza zoezi la kuwapokonya silaha raia

Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kuwa, inatarajia kuanza zozei la kuwapokonya silaha raia.

Taarifa zinasema kuwa, zoezi la kuwapokonya raia silaha kwa khiyari litaendehswa na jeshi la ulinzi la nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Jeshi la Sudan Kusini limesema litaanzisha zoezi la kukusanya silaha kutoka kwa vijana watakaokuwa tayari kusalimisha kwa khiyari katika maeneo ambayo yako chini ya sheria ya hali ya dharura.

Jeshi hilo limesema kuwa, baada ya zoezi hilo, utafuata mchakato wa kuwapokonya watu silaha kwa lazima utakaofanywa na kikosi maalumu katika kaunti za Warrap na Mayom, ambako wiki iliyopita Rais Salva Kiir alitangaza hali ya dharura kufuatia hofu ya usalama kwa kipindi cha miezi sita.

Maeneo hayo yanakabiliwa na ongezeko kubwa la machafuko ya kikabila yakihusisha wizi wa mifugo.

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Sudan Kusini, Lul Ruai Koang, amewaambia waandishi habari kuwa, tayari kikosi cha kusimamia zoezi la ukusanyaji silaha kimepelekwa kwenye maeneo hayo ili kutekeleza mpango huo.

Kukosekana utulivu wa kisiasa na kuongezeka vita na mapigano tangu mwishoni mwa mwezi Februari kati ya makundi yenye silaha ndani ya Sudan Kusini kumesababisha hali kuwa mbaya zaidi hasa katika jimbo la Upper Nile, lakini pia maeneo mengine ya Sudan Kusini maisha ni mabaya na huduma muhimu haziko.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) linasema kuwa, Sudan Kusini inaendelea kuwa moja ya nchi zenye matatizo makubwa zaidi ya wakimbizi katika eneo hilo, huku zaidi ya Wasudan Kusini milioni 2.3 wakiishi kama wakimbizi katika nchi za DRC, Ethiopia, Kenya, Uganda na Sudan.”