Rwanda: Nchi za Afrika zitumie teknolojia kuimarisha sekta ya kilimo
Waziri Mkuu wa Rwanda ametoa mwito kwa nchi za Afrika kukumbatia teknolojia na ubunifu kupiga jeki sekta ya kilimo barani humo.
Edouard Ngirente ametoa mwito huo katika hotuba yake ya ufunguzi wa Kongamano la Afrika Kuhusu Teknolojia za Kilimo jijini Kigali jana Jumanne.
Mkutano huo wa siku nne unaofanyika chini ya kaulimbiu "Suluhu za Kizazi Kijacho za Teknolojia za Kilimo kwa Wakulima wa Afrika" umewaleta pamoja washiriki 900, wakiwemo wanasayansi, wabunifu, wakulima na watungaji sera kutoka nchi za Afrika na duniani kote.
Waziri Mkuu wa Rwanda, Edouard Ngirente amesema washiriki wote wa mkutano huo wana jukumu la kuboresha na kuimarisha mustakabali wa kilimo barani Afrika.
Ameeleza bayana kuwa: Mustakabali huu unategemea mambo kadhaa, ikiwemo kuhakikisha wakulima wanapata vifaa na suhula wanazohitaji, teknolojia ya data za kuwatafutia masoko miongoni mwa mambo mengine.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, serikali za nchi za Afrika ziliihimizwa kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo ili kuimarisha usalama wa chakula na kufungua mustakbali wa maendeleo endelevu ya kiuchumi.
Katika mkutano huo wa siku tatu uliofanyika Nairobi, mji mkuu wa Kenya, wajumbe walisema ingawa sekta ya kilimo inaajiri asilimia 60 ya watu barani Afrika na kuchangia asilimia 23 ya Pato Ghafi la Taifa (GDP) kwa nchi za bara hilo, lakini bado sekta hiyo inaendelea kutengewa bajeti hafifu na kupata uwekezaji mdogo kuliko inavyohitajika.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Afrika Mashariki (IGAD), watu milioni 67.4 wa eneo la Pembe ya Afrika hawana uhakika (usalama) wa chakula.