WFP: Raia wa Kusini mwa Khartoum wanakabiliwa na tishio la njaa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i127462-wfp_raia_wa_kusini_mwa_khartoum_wanakabiliwa_na_tishio_la_njaa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP limeonya kuwa, maeneo kadhaa kusini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum yamo hatarini kukumbwa na baa la njaa, kutokana na kuendelea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
(last modified 2025-06-11T22:44:10+00:00 )
Jun 11, 2025 22:44 UTC
  • WFP: Raia wa Kusini mwa Khartoum wanakabiliwa na tishio la njaa

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP limeonya kuwa, maeneo kadhaa kusini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum yamo hatarini kukumbwa na baa la njaa, kutokana na kuendelea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Onyo hili la Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limetolewa, huku kukiwa na uhitaji mkubwa wa rasilimali nyingi, wakati huu WFP ikielezea kukumbwa na upungufu wa fedha za msaada wa chakula kwa mikoa iliyoharibiwa na vita.

Katika Mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva kwa njia ya video kutokea Port Sudan Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan, Laurent Bukera, ameeleza kuwa kiwango ch njaa na ufukara vimeenea katika sehemu nyingi za nchi hiyo zilizokumbwa na vita.

Bukera amesema raia wengi wamekuwa wakiishi bila ya matumaini wala matarajio ya kupata chakula, hali ambayo pia inasababisha maafa zaidi.

Haya yanajiri wakati Umoja wa mataifa umeendelea kutoa wito kwa Jumuiya za kikanda kuchangia katika juhudi za upatikanaji wa amani kwenye nchi hiyo. Idadi ya watu ambao wameikimbia Sudan tangu kuanza kwa vita vyake vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2023 ikipindukia milioni nne. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilisema hayo Jumanne na kuongeza kuwa, wengi wa walionusurika wanakabiliwa na makazi duni kutokana na uhaba wa fedha.

Vita hivyo vilivyoanza Aprili 2023, vimesababisha uharibifu mkubwa wa mali ya umma na miundombinu muhimu, kuua makumi ya maelfu ya watu, mbali na kulazimisha mamilioni kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.