England yaangushwa kwa mara ya kwanza na timu ya Afrika
(last modified Thu, 12 Jun 2025 07:42:20 GMT )
Jun 12, 2025 07:42 UTC
  • England yaangushwa kwa mara ya kwanza na timu ya Afrika

Timu ya taifa ya Senegal imeandika historia kwa kuichapa England mabao 3-1 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa Jumanne mjini Nottingham, Uingereza.

Hii ndiyo mara ya kwanza kwa England kupoteza mechi dhidi ya timu kutoka bara la Afrika. Ushindi huu pia unaifanya Senegal kuwa na rekodi ndefu zaidi ya kutopoteza mechi yaani michezo 22 mfululizo bila kipigo.

Gazeti la The Independent lilielezea mchezo huo kuwa ulikuwa wa "England kupitwa kwa pasi, kasi na maarifa" na wapinzani waliokuwa "wajanja na waliocheza kwa mpangilio mzuri zaidi."

England ilianza kwa kishindo dakika ya saba kupitia nahodha wao Harry Kane, ambaye alifunga bao lake la nne katika mechi nne mfululizo tangu kuwasili kwa kocha mpya, Thomas Tuchel. Kane sasa anakuwa mchezaji wa kwanza wa England kufunga bao katika kila moja ya mechi nne za kwanza za kocha mpya.

Senegal ilisawazisha dakika ya 40 kupitia Ismaila Sarr kabla ya Abib Diarra kuipa uongozi dakika ya 62. Bao la mwisho lililozika kabisa matumaini ya England lilifungwa na Cheikh Tidiane Sabaly katika dakika za nyongeza.

Ushindi huu wa kihistoria wa Simba wa Teranga umevunja rekodi ya England dhidi ya timu za Afrika, ambapo hapo awali walikuwa na ushindi 15 na sare 6, bila kupoteza hata mchezo mmoja. Pia ni mara ya pili tu kwa England kufunga bao la kwanza nyumbani na hatimaye kupoteza kwa tofauti ya mabao mawili, mara ya mwisho ilikuwa dhidi ya Brazil mwaka 1995.

Katika kipindi cha kwanza pekee, Senegal ilipiga mashuti sita yaliyolenga lango hiyo ikiwa idadi kubwa zaidi kuwahi kufanywa na timu yoyote dhidi ya England tangu Brazil ilipopiga mashuti manane mwaka 2013.

Hii ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa kocha Tuchel kupoteza tangu achukue mikoba ya kuinoa England, baada ya kuiongoza kupata ushindi dhidi ya Albania, Latvia na Andorra.

Senegal, mabingwa wa Afrika, wanaendelea kujiandaa kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2025, huku England wakijiweka tayari kwa mechi za kufuzu Kombe la Dunia la 2026.