China, Afrika zaitaka Marekani kutatua mvutano wa kibiashara kwa mazungumzo yenye usawa
(last modified Thu, 12 Jun 2025 07:48:01 GMT )
Jun 12, 2025 07:48 UTC
  • China, Afrika zaitaka Marekani kutatua mvutano wa kibiashara kwa mazungumzo yenye usawa

Nchi 53 za Afrika pamoja na China zimeitaka Marekani kurejea kwenye meza ya mazungumzo ya kibiashara kwa msingi wa “usawa, heshima na manufaa ya pande zote”. Pia zimeihimiza kuachana na ushuru wa kulinda bidhaa za ndani na badala yake kuzingatia majadiliano ya kimataifa ya pande nyingi.

Wito huo umetolewa kupitia Tamko la Changsha la Ushirikiano wa China na Afrika kwa Ajili ya Mshikamano wa Kusini - Kusini, lililotangazwa katika mkutano wa mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mjini Changsha, mji mkuu wa mkoa wa Hunan katikati mwa China.

Tamko hilo limesema: “Kutokana na baadhi ya mataifa kujaribu kuvuruga utaratibu wa sasa wa uchumi na biashara ya kimataifa kwa ushuru wa kulinda bidhaa za ndani, jambo linalohatarisha maslahi ya jumuiya ya kimataifa, tunatoa wito kwa mataifa yote, hususan Marekani, kurejea kwenye njia sahihi ya kutatua mivutano ya kibiashara kupitia mashauriano yanayoendeshwa kwa misingi ya usawa, heshima na manufaa ya pande zote.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, pamoja na mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi kadhaa za Afrika na maafisa waandamizi walihudhuria mkutano huo.

Tamko hilo lenye vipengele 10 linasisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa inapaswa kuipa Afrika kipaumbele katika changamoto zake za kiuchumi, likisisitiza kuwa misaada ya maendeleo “inapaswa kuongezwa kwa ufanisi na si kupunguzwa kwa uamuzi wa upande mmoja,” na likatoa wito wa “uendeshaji halisi wa mfumo wa kimataifa wa pande nyingi.”

Tamko hilo pia lilionya kuwa “utekelezaji wa sera za upande mmoja, ulinzi wa bidhaa za ndani, na unyanyasaji wa kiuchumi” ni changamoto kubwa kwa bara la Afrika na mataifa mengine ya Kusini mwa dunia.

China imetangaza kuwa iko tayari kupanua sera yake ya ushuru wa sifuri kwa bidhaa kutoka nchi zote 53 za Afrika zinazotambua uhusiano wa kidiplomasia na Beijing – isipokuwa Eswatini – ili kusaidia kuimarisha mauzo ya bidhaa za Afrika.

Takwimu kutoka Idara Kuu ya Forodha ya China, kama ilivyoripotiwa na Global Times, zinaonyesha kuwa thamani ya biashara kati ya China na Afrika ilipanda hadi yuan trilioni 2.1 (sawa na dola bilioni 292) mwaka 2024, ikilinganishwa na chini ya yuan bilioni 100 (dola bilioni 13.9) mwaka 2000.

Wito huu wa mazungumzo ya usawa umetolewa wakati ambapo mvutano kati ya Marekani na mataifa kadhaa ya Afrika kuhusu hatua za kibiashara unaendelea kuongezeka. Mwezi Aprili, Washington iliweka ushuru mkubwa kwa bidhaa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, ikiwa ni pamoja na asilimia 50 kwa bidhaa kutoka Lesotho, asilimia 47 kutoka Madagascar, asilimia 40 kutoka Mauritius, asilimia 38 kutoka Botswana, na asilimia 31 kutoka Afrika Kusini.

Pembeni mwa mkutano huo, Wang Yi alikutana na mawaziri wa mambo ya nje kutoka Kenya, Senegal, Tanzania, Namibia, Botswana na Angola kujadili masuala ya biashara, uwekezaji na ushirikiano wa maendeleo.