Rais Traore: Mabeberu wanajaribu kuvunja Muungano wa Sahel
(last modified Thu, 12 Jun 2025 07:52:41 GMT )
Jun 12, 2025 07:52 UTC
  • Rais Traore: Mabeberu wanajaribu kuvunja Muungano wa Sahel

Rais wa mpito wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, amezishutumu nchi za kigeni kwa kujaribu kuhujumu Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES) kwa kuwachochea wanachama kusalitiana.

Akizungumza katika sherehe ya kuinua bendera ya taifa, Traoré amesema kuwa Muungano wa Mataifa ya Sahel umeendelea kuwa “chanzo cha wasiwasi” kwa mabeberu.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Habari la Burkina Faso, Traore amesema: “Kila siku tunachochewa na mabeberu wanaotaka kulazimisha moja ya mataifa matatu kusaliti wenzao.” Ameongeza kuwa, “Tumezoea hali hii kwa muda sasa. Kila mara ni njama ya kujaribu kuvunja mshikamano wetu. Hili linapaswa kutufikirisha kwa kina.”

Muungano wa Mataifa ya Sahel  ulianzishwa rasmi Septemba 2023 na Burkina Faso, Mali, na Niger kama mkataba wa pamoja wa ulinzi na ushirikiano baada ya kuondolewa kwa wanajeshi wa Ufaransa katika mataifa hayo. Tangu wakati huo, nchi hizo zinazoongozwa na serikali za mpito za kijeshi zimejiondoa kutoka jumuiya ya ECOWAS, zikiitaja kuwa chombo cha ushawishi wa mkoloni wa zamani, Ufaransa, na tishio kwa uhuru wao.

Muungano wa Mataifa ya Sahel umejiweka kama upinzani thabiti dhidi ya ushawishi wa Magharibi katika ukanda wa Sahel, hususan dhidi ya mkoloni mkongwe, Ufaransa. Kikundi hicho pia kimesitisha ushirikiano wa kijeshi na washirika wao wa zamani wa Ulaya na Marekani na kuelekeza ushirikiano zaidi kwa Russia na washirika wengine wa nje ya ulimwengu wa Magharibi.

Katika wiki za hivi karibuni, maafisa wa serikali za Ouagadougou na Niamey pia wameishutumu Ufaransa na Ukraine kwa kufadhili ugaidi kwa lengo la kudhoofisha serikali za kijeshi za Sahel.

Mwisho wa mwezi uliopita, kiongozi wa mpito wa Niger, Jenerali Abdourahamane Tchiani, aliituhutumu Ufaransa kwa kushirikiana na waasi katika maeneo ya mipaka ya Benin na Nigeria, na kusema kuwa ni sehemu ya mpango wa kuuvuruga usalama wa Niger na ukanda mzima wa Sahel. Ukraine pia imetajwa kwa madai ya kuhusika katika kutekeleza ajenda chafu ya mataifa ya Magharibi kwa kutoa mafunzo na silaha kwa waasi walioko nyuma ya zaidi ya muongo mmoja wa ghasia za kijihadi nchini Mali.

Rais wa Burkina Faso, Kapteni Traoré, ameonya kuwa juhudi za Magharibi za kuichafua Sahel zinaendeshwa na tamaa ya rasilimali lukuki za asili ambazo bado hazijagunduliwa wala kutumika ipasavyo.