Karibu watu 50 waaga dunia kwa mafuriko nchini Afrika Kusini
Watu karibu 50 wakiwemo wanafunzi wa Shule, wamepoteza maisha Nchini Afrika Kusini kutokana na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kwenye mkoa wa Cape Mashariki.
Mkuu wa mkoa huo, Oscar Mabuyane amesema kuwa, hali inaendelea kuwa mbaya na kuna uwezekano mkubwa wa idadi ya vifo kuongezeka. Taarifa zaidi zinasema kuwa, wanafunzi wanne wa shule na dereva wao ni miongoni mwa watu walipoteza maisha, baada ya basi lao kusombwa na maji ya mafuriko.
Manusura kadhaa waliokolewa baada ya kukimbilia juu ya paa au kwenye miti. "Mvua zisizokwisha, upepo mkali, na maporomoko ya ardhi yamesababisha vifo vya watu kadhaa na kusababisha uharibifu mkubwa," anasema mkuu wa serikali ya eneo hilo. Mamia ya watu wamelazimika kupewa hifadhi katika makazi ya dharura baada ya nyumba zao kujaa maji.
Mbali na maafa, mamia ya watu wameachwa bila makaazi, na kuwalazimu kujenga makaazi ya muda kipindi hiki cha mvua kubwa.
Wizara ya elimu inasema shule 58 zimeathiriwa, katika mkoa wa Cape Mashariki, huku zingine zaidi ya 60 katika wilaya tisa katika mkoa wa KwaZulu-Natal, zikiharibiwa.
Mbali na mafuriko, wakaazi wa mkoa huo pia kuanzia wiki hii, wanashuhudia baridi kali na upepo mkali na kuwaacha watu zaidi ya 500, bila umeme.
Mamlaka husika nchini Afrika Kusini zimetangaza kuwa, operesheni za uokoaji na utoaji misaada zinaendelea kuhakikisha walioathirika wanafikiwa na misaada.