Takriban Wasudan 75,000 wamekimbia Ethiopia kutafuta usalama wao
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi limetangaza kuwa, takriban Wasudan 75,000 wamekimbia Ethiopia kutafuta usalama wao tangu mgogoro wa uchu wa madaraka baina ya majenerali ulipozuka nchini humo zaidi ya miwili iliyopita.
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), amesema katika katika taarifa yake ya hivi karibuni kuhusu harakati za watu kutoka Sudan kwenda Ethiopia kwamba, serikali ya Ethiopia imepokea maelfu ya watu waliokimbia makazi yao katika maeneo mbalimbali ya Sudan hasa ya mpakani mwa Ethiopia, tangu majenerali wa kijeshi walipozozana na kuingia vitani nchini Sudan mwezi Aprili 2023.
Kwa mujibu wa UNHCR, kati ya wakimbizi 74,142 waliofika Ethiopia, 44,156 ni raia wa Sudan, 19,490 ni raia wa Ethiopia waliorejea kwao na 10,496 ni wa nchi nyingine.
"Huku mzozo ukiendelea nchini Sudan, takriban wakimbizi 6,355 wamevuka mpaka na kuingia Ethiopia tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2025," imebainisha taarifa hiyo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
UNHCR imeongeza kuwa, kutokana na kuongezeka idadi ya wakimbizi wanaoingia Ethiopia, hasa kutoka nchi jirani ya Sudan, Ethiopia sasa inakuwa ni nchi ya tatu barani Afrika yenye wakimbizi wengi na inakadiriwa kuwa, sasa hivi kuna wakimbizi zaidi ya milioni 1 waliosajiliwa na wasiosajiliwa ambao wamekimbilia nchini humo kutokana na ukosefu wa usalama katika nchi zao.