Afrika Kusini yalaani mashambulizi ya kigaidi ya Israel dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i127556-afrika_kusini_yalaani_mashambulizi_ya_kigaidi_ya_israel_dhidi_ya_iran
Afrika Kusini usiku wa kumkia leo Jumamosi imelaani mashambulizi ya kigaidi ya Israel dhidi ya Iran na kuhimiza kufanyika juhudi za kidiplomasia za kupunguza mivutano katika eneo la Asia Magharibi.
(last modified 2025-06-14T07:20:08+00:00 )
Jun 14, 2025 07:20 UTC
  • Afrika Kusini yalaani mashambulizi ya kigaidi ya Israel dhidi ya Iran

Afrika Kusini usiku wa kumkia leo Jumamosi imelaani mashambulizi ya kigaidi ya Israel dhidi ya Iran na kuhimiza kufanyika juhudi za kidiplomasia za kupunguza mivutano katika eneo la Asia Magharibi.

Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano ya Afrika Kusini (DIRCO) imesema katika taarifa yake iliyotolewa Ijumaa usiku kwamba: "Afrika Kusini inaelezea wasiwasi wake mkubwa kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na Israel ndani ya Iran tarehe 13 Juni 2025, ikiwa ni pamoja na athari za mashambulizi hayo kwenye maeneo ya kijeshi, vituo vya nyuklia na miundombinu ya kiraia. Ripoti za raia kujeruhiwa pamoja na wanajeshi, zinasumbua sana."

"Hatua hizi zinazua wasiwasi mkubwa mbele ya sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na sheria za uhuru, uadilifu na ulinzi wa raia zilizoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa za kibinadamu," imesema sehemu nyingine ya taaarifa ya idara hiyo ya Afrika Kusini.

Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano ya Afrika Kusini (DIRCO) pia imebainisha kuwa, Afŕika Kusini ina wasiwasi hasa kuhusu madhaŕa ya usalama wa maeneo ya nyuklia kutokana na mashambulio katika maeneo ya karibu na vituo vya nyuklia. 

Wakati ikitoa salamu zake za rambirambi kwa serikali ya Iran na familia za watu wote waliouawa shahidi katika hujuma ya kigaidi ya Israel; Afrika Kusini pia imetilia mkazo msimamo wake usioyumba wa kutatuliwa kwa amani mizozo yote.

"Tunaunga mkono majadiliano ya pande mbili kati ya Iran na Marekani na juhudi za kuifanya Asia Magharibi kuwa eneo lisilo na silaha za nyuklia," imeongeza taarifa hiyo.